Madaktari bingwa na watoa huduma za afya zaidi ya 450 kutoa matibabu ya bure siku 7 arusha

Madaktari Bingwa na Watoa huduma za afya zaidi ya 450 kutoka kwenye Hospitali na Taasisi takribani 40 za afya Nchini wanatarajiwa kutoa huduma za vipimo na matibabu bure kwa Wakazi wa Mkoa wa Arusha kwa siku saba mfululizo kuanzia Jumatatu ya wiki ijayo June 24, 2024.


Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Christian Makonda amesema hayo leo June 22,2024 mara baada ya kukagua maandalizi ya kliniki hiyo ya afya inayotarajiwa kuzinduliwa Jumatatu ya wiki ijayo kwenye viwanja vya michezo vya Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha.

Makonda ametumia nafasi hiyo kuwakaribisha Wananchi wote wa Arusha kujitokeza kwa wingi kwenye kliniki hiyo, akitoa hakikisho la vipimo, matibabu na dawa bure kwa kila Mwananchi atakayebanika na kugundulika kuwa na magonjwa na maradhi ya aina mbalimbali.

“Ndugu zangu asiwaambie Mtu, kwenye suala la afya kuna Watu wameuza nyumba zao, wameuza viwanja, wamefilisika biashara zao katika kupambana kuuguza Ndugu zao na kuna nyakati nyingine kuna Ndugu zetu wameshindwa hata kukomboa miili ya Ndugu zao kutokana na madeni ya gharama za matibabu, neema hii ambayo Mungu ametupa tukaitumie na mikono ya watumishi wa Mungu ikafungue baraka ili tukapate afya kupitia madaktari wetu hawa Bingwa”

Makonda amesema Hospitali na Taasisi zitakazoshiriki kwenye kliniki hiyo na kutoa Madaktari ni pamoja na Hospitali ya Taifa Muhimbili, Hospitali ya Afya ya Akili Mirembe, Hospitali ya kanda KCMC, Hospitali ya Kanda Benjamin Mkapa, Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Taasisi ya mifupa Moi pamoja na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Hospitali ya Mawenzi pamoja na Hospitali na Taasisi nyingine za ndani na nje ya Mkoa wa Arusha.

Share: