Jeshi la Polisi tayari linayashikilia magari hayo kwenye kituo kikuu cha Polisi wa usalama barabarani
Jeshi la Polisi mkoani Arusha limesema lipo tayari kushirikiana na Mkuu wa Mkoa na wakuu wa wilaya zote za Mkoa wa Arusha kwenye kuhakikisha haki za wananchi zilizopotea zinapatikana kwa haraka kulingana na maelekezo yatakayotolewa.
Kamanda wa Polisi mkoani Arusha Kamishna msaidizi mwandamizi wa Polisi Justine Masejo ametoa taarifa hiyo wakati alipokuwa akizungumzia utekelezaji wa maagizo mbalimbali ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda, yaliyotokana na kliniki yake ya kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wananchi iliyofanyika Mei 8-10 mwaka huu.
Kamanda wa Polisi amesema miongoni mwa kesi walizozishughulikia ni pamoja na ukamataji wa magari ya kubeba mizigo yanayomilikiwa na wanandoa wa zamani yaliyokuwa yanaharibiwa na kuuzwa kwa spea na aliyekuwa Mume wa Mwalimu Sabina John Mosi.m
Mei 08, 2024 Mwalimu Sabina alifika Mbele ya Mkuu wa Mkoa na kumueleza kuwa wakati wa mahusiano yake na Julius Mwase walifanikiwa kuwa na mali kadhaa ikiwemo nyumba na magari na baada ya kutengana aliyekuwa mume wake alianza kuuza spea za magari waliyokuwa wanamiliki kinyume na sheria na taratibu za umiliki.
Baada ya kusikilizwa, Mhe. Mkuu wa Mkoa aliliamuru Jeshi la Polisi kushikilia magari hayo wakati wakisubiri kusikilizwa kwa shauri la madai ambalo limepelekwa mahakamani na Mwalimu Sabina.
Jeshi la Polisi tayari linayashikilia magari hayo kwenye kituo kikuu cha Polisi wa usalama barabarani na Kamanda Masejo anasema wanasubiri maamuzi ya Mahakama na kile ambacho watakiamua kuhusu umiliki wa magari hayo.