M23 wakaribisha usitishaji vita uliosimamiwa na marekani

Kundi la waasi la M23 limekubali kuheshimu makubaliano ya siku tatu ya kusitisha mapigano yaliyosimamiwa na Marekani na jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Msemaji wa kundi hilo, Lawrence Kanyuka, alisema katika taarifa yake kwenye mtandao wa X (zamani Twitter) kwamba waasi walikubali mpango huo "kwa kuwa unaendana na makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyotiwa saini na M23 ya tarehe 7 Machi 2023".

Kundi hilo la waasi halikuwa limeshauriana kuhusu mpango huo kabla ya kukamilika mashauriano, kulingana na Bw Kanyuka.

Licha ya kukubaliana na usitishaji mapigano, M23 walisema "hawatasita" kujilinda - na raia walio chini ya udhibiti wao - kutoka kwa jeshi au wanamgambo wanaoungwa mkono na serikali.

Usitishwaji wa mapigano ulianza Jumatatu adhuhuri, kwa mujibu wa taarifa ya Msemaji wa Baraza la Usalama la Kitaifa la Marekani Adrienne Watson.

Haya yanajiri wakati kikosi cha kulinda amani cha Afrika Mashariki kikiondoa wanajeshi wake kutoka DR Congo baada ya serikali kukataa kurejesha mamlaka yake.

Makubaliano ya hapo awali ya kusitisha mapigano yamekiukwa, na kusababisha mapigano mapya kati ya jeshi na waasi.

Share: