Liberia: george weah atangaza kutokugombea urais

Rais anayemaliza muda wake wa Liberia George Weah amesema hana mpango wa kutaka kuchaguliwa tena mwaka 2029 baada ya kushindwa katika uchaguzi wa hivi majuzi.

Bw Weah, mwanasoka wa zamani wa kimataifa, alichaguliwa mwaka wa 2017 lakini akashindwa katika uchaguzi wa Novemba na Joseph Boakai, ambaye anatazamiwa kuapishwa Jumatatu.

Akihutubia waumini wa kanisa siku ya Jumapili viungani mwa mji mkuu Monrovia, Bw Weah alisema atakuwa na umri wa miaka 63 baada ya miaka sita, na hatakuwa tayari kujihusisha na siasa zaidi ya miaka 65.

“Nina miaka 57 sasa na umri wetu wa kustaafu ni miaka 65 na miaka sita kuanzia sasa nitakuwa 63 na siwezi kufanya kazi kwa miaka miwili,” alisema.

Bw Weah alisema alihitaji "wakati kwa ajili yangu, watoto na familia".

“Sikuja kwenye siasa ili kuchukua mamlaka.Hamtanivuta kwenye siasa hadi nifikishe miaka 90,” aliongeza.

"Nasema asanteni Waliberia kwamba nimekuwa rais iwe mara moja au mara 50, lakini ninaweza kuwahakikishia kuwa ni mara moja."

Hakufichua alichopanga kufanya baadaye lakini alisema atahimiza amani na ustawi katika nchi yake.

Katika hotuba yake iliyosifiwa na watu wengi mwezi Novemba, Bw Weah alisema chama chake cha Congress for Democratic Change (CDC) kitasalia kuwa upinzani mkali.

Share: