Lalit Patidar Avunja rekodi binadamu mwenye nywele nyingi usoni

Lalit Patidar, Kijana wa miaka 18 nchini India ameweka historia kwa kutwaa rekodi ya dunia ya Guinness ya kuwa na uso wenye nywele nyingi zaidi kwa mwanamume.

Lalit Patidar ana karibu nywele 202 kwa kila sentimita ya mraba kwenye uso wake kutokana na hali adimu inayoitwa hypertrichosis, au "werewolf syndrome".

Licha ya kutumbuliwa macho na wanafunzi wenzake alipokuwa mtoto, kijana huyo kutoka jimbo la kati la Madhya Pradesh aliiambia Guinness World Records kwamba anakubali upekee wake na sasa anashiriki machache ya maisha yake ya kila siku kwenye chaneli yake ya YouTube.

Hivi majuzi, kijana huyo alisafiri kwenda Milan kwa Lo Show dei Record, ambapo rekodi yake ilithibitishwa rasmi. Zaidi ya asilimia 95 ya uso wake umefunikwa na nywele.

"Lalit ni mmoja kati ya visa 50 vilivyoripotiwa kote ulimwenguni tangu Enzi za Kati, na kumfanya kuwa mmoja kati ya bilioni," Guinness World Records ilisema kwenye tovuti yake.

"Ni nadra sana kwamba watu hawanitendei vizuri. Watu wengi ni wema kwangu. Inategemea mtu. Siku ya kwanza shuleni haikuwa nzuri sana kwa sababu watoto wengine waliniogopa, lakini waliponijua, waligundua kwamba sikuwa tofauti sana nao.”

Baada ya kupokea jina hilo, alisema: “Sina la kusema. Sijui niseme nini kwa sababu nina furaha sana kupata kutambuliwa hivi.”

Ingawa baadhi ya watu wanamsihi aondoe nywele zake usoni, yeye anajibu kwa ujasiri kwamba anajipenda jinsi alivyo. "Ninapenda jinsi nilivyo, na sitaki kubadilisha sura yangu."

Share: