Kundi la g7 limekubali kutumia mali ya urusi iliyokamatwa ya takriban $50bn (£39bn) kwa ukraine

Kundi la G7 limekubali kutumia mali ya Urusi iliyokamatwa ya takriban $50bn (£39bn) kwa Ukraine kuisaidia kupambana na majeshi ya Urusi yanayovamia.

Rais wa Marekani Joe Biden amesema ni ukumbusho mwingine kwa Urusi "kwamba haturudi nyuma", lakini Moscow imetishia hatua "zinazoumiza sana" za kulipiza kisasi.

Pesa hizo hazitarajiwi kufika hadi mwisho wa mwaka lakini zinaonekana kuwa suluhu la muda mrefu la kuunga mkono juhudi za vita na uchumi wa Ukraine.

Pia katika mkutano wa kilele wa G7 nchini Italia, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky na Bw Biden walitia saini mkataba wa miaka 10 wa usalama kati ya Ukraine na Marekani, uliopongezwa na Kyiv kama "wa kihistoria".

Makubaliano hayo yanatazamia msaada wa kijeshi wa Marekani na mafunzo kwa Ukraine - lakini haitoi ahadi ya Washington kutuma wanajeshi kupigania mshirika wake.

Baadhi ya mali zenye thamani ya $325bn zilizuiliwa na G7, pamoja na EU, kufuatia uvamizi kamili wa Urusi nchini Ukraine mnamo 2022.

Chungu cha mali hiyo kinazalisha takriban $3bn kwa mwaka za faida.

Chini ya mpango wa G7, $3bn zitatumika kulipa riba ya kila mwaka ya mkopo wa $50bn kwa Waukraine, uliotolewa kwenye masoko ya kimataifa.

Akizungumza katika mkutano wa pamoja wa wanahabari kwenye ukumbi wa mkutano huo huko Puglia, kusini mwa Italia, Rais Biden alisema mkopo huo wa $50bn "utawasaidia Ukraine na kumkumbusha [Rais wa Urusi Vladimir] Putin kwamba hatusalimu amri. ".

Kiongozi huyo wa Marekani alisisitiza kuwa Bw Putin "hawezi kutusubiri, hawezi kutugawa, na tutakuwa pamoja na Ukraine hadi washinde katika vita hivi".

Rais Zelensky aliwashukuru Wamarekani na washirika wake wengine kwa msaada wao

Share: