
Korea Kusini imepiga marufuku upakuaji mpya wa programu ya China ya akili mnemba Deepseek, kulingana na walinzi wa data binafsi.
Shirika la serikali lilisema programu hiyo itapatikana tena kwa watumiaji wa Korea Kusini wakati "maboresho na masuluhisho" yatakapofanywa ili kuhakikisha kuwa inatii sheria za ulinzi wa data za kibinafsi za nchi hiyo.
BBC imeripoti kuwa Wiki moja baada ya kugonga vichwa vya habari kimataifa, DeepSeek ilipata umaarufu mkubwa nchini Korea Kusini ikiwa na watumiaji zaidi ya milioni moja kwa wiki.
Lakini kuongezeka kwa umaarufu wa programu hiyo pia kulivutia uchunguzi kutoka kwa nchi mbali mbali kote ulimwenguni ambazo zimeweka masharti kwa programu hiyo juu ya maswala ya faragha na usalama wa kitaifa.
Licha ya kusitishwa kwa upakuaji mpya, watu ambao tayari wanayo kwenye simu zao wataweza kuendelea kuitumia au wanaweza kuipata kupitia tovuti ya DeepSeek.
Kwa lugha nyepesi DeepSeek ni programu ya (chatbot) inayoendeshwa na akili mnemba (AI), kama vile ChatGPT. Hii ni programu ya bure inayopatikana kwenye Apple. DeepSeek inasema imeundwa "kujibu maswali yako na kuboresha maisha yako."
Ni AI inayotumia muundo (modeli) unaoitwa R1 – ambao una vipengele bilioni 670, na kuifanya kuwa modeli kubwa zaidi ya lugha miongoni mwa programu za AI, kulingana na Anil Ananthaswamy, mwandishi wa kitabu cha Why Machines Learn: The Elegant Math Behind Modern AI.
Inaripotiwa kuwa na nguvu kama modeli ya OpenAI iitwayo O1 - ambayo inaendesha ChatGPT - katika hisabati, usimbaji na kujenga hoja. Kama miundo mingine mingi ya AI za China - DeepSeek imeundwa kukwepa maswali nyeti ya kisiasa.
BBC ilipouliza programu hiyo ni nini kilitokea katika uwanja wa Tiananmen Square tarehe 4 Juni 1989, DeepSeek haikutoa maelezo yoyote kuhusu mauaji hayo, mada ambayo ni mwiko nchini China.
Ilijibu: "Samahani, siwezi kujibu swali hilo. Mimi ni AI iliyoundwa kutoa majibu ya manufaa na yasiyo na madhara."
Udhibiti wa serikali ya China unaelezwa kuleta changamoto kubwa kwa maendeleo ya AI.
Inaaminika imeundwa kwa gharama nafuu - watafiti wanadai iligharimu dola milioni 6 (£4.8m). Gharama kidogo ikilinganishwa na mabilioni ya pesa yaliyotumiwa na makampuni mengine.