Kasi ya kimbunga hidaya yazidi kusogelea pwani ya tanzania

Mienendo ya mifumo ya hali ya hewa baharini bado inaonyesha uwezekano mkubwa wa Kimbunga Hidaya kuendelea kusogea karibu na pwani ya Tanzania na kuendelea kuwepo hadi tarehe sita mwezi Mei 2024, kwa mujibu wa Mamlaka ya hali ya Hewa Tanzania TMA.

Kulingana na mamlaka hiyo, kimbunga hicho kinaendelea kuimarika na kwamba hadi kufikia usiku wa kuamkia leo kasi yake ilikuwa imeimarika na kufikia kilomita 110 kwa saa.

Taarifa hiyo inasema kwamba kimbunga hicho kitaendelea kuimarika na kuwa kikubwa zaidi katika saa 24 zijazo.

Imesema kwamba uwepo wa kimbunga hicho katika pwani ya Tanzania utavuruga mifumo ya ali ya hewa nchini na kusababisha mvua kubwa na upepo mkali.

Baadhi ya maeneo yatakayoathirika sana ni Mikoa ya Mtwara, Dar es Salaam, Lindi, maeneo ya Tanga, Morogoro , visiwa vya pemba na Unguja pamoja na maeneo Jirani.

Taarifa hiyo imeongezea kwamba tayari vipindi vya mvua nyepesi na upepo wa wastani vimeanza kujitokeza katika maeneo ya Mtwara.

TMA imesema kwamba ongezeko la mvua na upepo mkali utakaoambatana na mawimbi makubwa baharini vinatarajiwa kusambaa katika maeneo mengi ya ukanda wa pwani kuelekea tarehe 4 hadi 6 mwezi Mei 2024.

Kutokana na hilo, TMA imetoa tahadhari kwa wananchi katika maeneo husika na wote wanaojihusisha na shuguli mbalimbali baharini .

VIlevile Mamlaka hiyo imewataka Watanzania kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiriwa hali ya Hewa.









Share: