Jumla ya walimu wakuu 20,661 wamepewa mafunzo ya utekelezaji wa mitaala ya elimu iliyoboreshwa mwaka 2023

Jumla ya Walimu Wakuu 20,661 wa Shule za Msingi za Serikali na Sizizo za serikali nchini wamepewa mafunzo kuhusu utekelezaji wa mitaala ya Elimu ya Awali na Msingi iliyoboreshwa mwaka 2023.


Akizungumzia hitimisho la mafunzo hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dkt. Aneth Komba amesema kuwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais-TAMISEMI kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania imekamilisha kazi ya utoaji wa mafunzo hayo yaliyoanza tarehe 5 Mei, 2024, na kuhitimishwa tarehe 12 Juni, 2024 katika mikoa 26 ya Tanzania Bara.

Ameeleza kuwa lengo la Mafunzo lilikuwa ni kuwajengea uelewa wa pamoja wakuu hao kuhusu mabadiliko ya Mtaala wa Elimu ya Awali na Msingi wa Mwaka 2023 ili waweze kusimamia, kutekeleza na kufanya ufuatiliaji kwa ufanisi, huku akiishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais, Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kugharamia mafunzo hayo.

“Kwanza namshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano , Mhe, Dkt Samia Suluhu Hassan kupitia wizara za Elimu, Sayansi na Teknolojia na OR-TAMISEMI kuwezesha kufanyika kwa mafunzo hayo kwani uwekezaji uliofanyika ni mkubwa ambapo tuna imani walimu wakuu hawa watakwenda sasa kutekeleza mtaala huu ulioboreshwa kama ulivyokusudiwa “alisema Dkt.Komba.

Share: