Assange alishikiliwa kwa miaka mitano iliyopita katika gereza la Uingereza, ambako alikuwa akipambana dhidi ya kurejeshwa Marekani.
Baada ya sakata ya kisheria iliyodumu kwa miaka mingi, Wikileaks inasema mwanzilishi wake Julian Assange ameondoka Uingereza baada ya kufikia makubaliano na mamlaka za Marekani ambayo yatamfanya akiri mashtaka ya jinai na kuachiwa huru.
Assange, 52, alishtakiwa kwa kula njama kupata na kufichua habari za ulinzi wa taifa.
Kwa miaka mingi, Marekani imekuwa ikisema nyaraka za Wikileaks - ambazo zilifichua taarifa kuhusu vita vya Iraq na Afghanistan - zilihatarisha maisha.
Assange alishikiliwa kwa miaka mitano iliyopita katika gereza la Uingereza, ambako alikuwa akipambana dhidi ya kurejeshwa Marekani.
Kulingana na CBS, mshirika wa BBC wa Marekani, Assange hatatumikia muda wowote chini ya ulinzi wa Marekani kama sehemu ya makubaliano na wizara ya sheria na atapewa msamaha kwa muda aliokaa jela nchini Uingereza.
Assange atarejea Australia, kulingana na barua ya wizara ya sheria. Kwenye mtandao wa X, jukwaa lililokuwa likijulikana kama Twitter, Wikileaks ilisema Assange aliondoka jela ya Belmarsh siku ya Jumatatu baada ya kukaa humo siku 1,901 katika seli ndogo.
Kisha "aliachiwa katika uwanja wa ndege wa Stansted wakati wa mchana, ambapo alipanda ndege na kuondoka Uingereza" kurejea Australia, taarifa hiyo iliongeza.
Video iliyosambazwa mtandaoni na Wikileaks inamuonyesha Assange, akiwa amevalia suruali ya jeans na shati la bluu, akipelekwa Stansted kabla ya kupanda ndege.