Jukumu la kurejesha amani mashariki ya congo lahamia sadc

Vikosi vya SADC vinachukua nafasi ya majeshi ya kulinda amani kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACRF) ambayo yamemaliza muda wake.

Hii ni baada ya majeshi ya kulinda amani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kumaliza muda wake.

Majeshi ya kulinda amani kutoka Jumuiya ya Kusini mwa Afrika (SADC) yameingia Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, tayari kwa jukumu la kurejesha amani eneo hilo.

Vikosi vya SADC vinachukua nafasi ya majeshi ya kulinda amani kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACRF) ambayo yamemaliza muda wake.

Akizungumza mara baada ya kupokea bendera kutoka kwa Kamanda wa EACRF Aphaxard Kiugu, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Peter Mathuki amesisitiza kuwa EAC itaendelea kuimarisha uwezo wake wa kukabiliana na changamoto za amani na usalama katika nchi wanachama ikiwa ni pamoja na kuunda sera, miongozo, mifumo na vyombo vinavyozingatia kanuni bora za kimataifa.

Katibu Mkuu huyo, pia aliupongeza uhodari, ushupavu na ujasiri uliooneshwa na EACRF wakati wote wa kulinda amani katika eneo hilo, akisema kazi hiyo ilikuwa ni ya mafanikio pamoja na changamoto zilizojitokeza.

Jukumu la EACRF nchini Congo lilitamatika Disemba 21, 2023 huku vikosi vya SADC vikiingia Mashariki ya Congo hivi karibuni. 

Kikosi hicho kiliundwa na wanajeshi kutoka Kenya, Uganda, Burundi na Sudan Kusini, na kutumwa mashariki mwa DRC mwishoni mwa mwaka 2022, kusaidia kuleta amani.

Hata hivyo, Serikali ya nchi hiyo ilivishutumu vikosi hivyo kwa kushindwa kuwakabili waasi wa M23.

Share: