Aidha, kama sehemu ya misheni hiyo, Jopo hilo la POE lilipata fursa ya kutembelea vituo kadhaa vilivyopo katika jiji la Kishasa na kushuhudia zoezi la upigaji kura lilivyofanyika.
Kufuatia maelekezo ya Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama (Organ of Troika) ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kwa Jopo la Wazee wa SADC (SADC Panel of Elders-POE), Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye ni Mwenyekiti wa Jopo hilo yupo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kushiriki Misheni ya SADC kwenye uchaguzi wa nchi hiyo unaofanyika tarehe 20 Desemba 2023.
Misheni hiyo ya SADC katika Uchaguzi Mkuu wa DRC inafanyika kufuatia mapendekezo ya Baraza la Ushauri wa Masuala ya Uchaguzi la SADC (SADC Electoral Advisory Council) kuwa katika uchaguzi huo wa DRC, SADC ipeleke Timu ya Uangalizi Uchaguzi (SADC Election Observation Mission, SEOM) sambamba na Jopo la Wazee (POE).
Timu ya Uangalizi wa Uchaguzi ya SADC inaongozwa na Makamu wa Rais Mstaafu wa Zambia Enock P. Kavindele, kwa kuwa Zambia ndiyo Mwenyekiti wa sasa wa Organ hiyo ya Troika. Timu hiyo ya SEOM inafanya majukumu ya kawaida ya uangalizi uchaguzi kama ilivyo utaratibu wa kawaida na SADC.
Kwa upande wake, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete anaongoza ujumbe huo wa POE unaojumuisha wajumbe wawili wa Kundi la Wapatanishi (Mediation Reference Group) ambao ni Lucy Mungoma, Katibu Mkuu Mstaafu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Zambia na Balozi na Balozi Joey, Katibu Mkuu Mstaafu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Zimbabwe pamoja na timu ya wataalamu kutoka Sekretarieti ya SADC.
Pamoja na mambo mengine, Jopo hilo la Wazee limepewa jukumu la kukukutana na kuzungumza na wadau mbalimbali katika uchaguzi huo wa DRC kwa lengo la kubaini na kutoa ushauri kuhusu maeneo yenye changamoto yanayoweza kupelekea kutokea kwa machafuko kabla, wakati na baada ya uchaguzi.
Rais Mstaafu Dkt Jakaya Kikwete na ujumbe wake walikutana na kufanya mazungumzo na viongozi na wadau kadhaa wa uchaguzi huo wakiwemo Denis Kadima, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Kongo (CENI), Martin Fayulu, Mgombea Urais wa Chama cha Engagement for Citizenship and Development Party (ECIDE), Denis Mukwege, Mgombea Binafsi wa Urais, pamoja na Franck Diongo, Kiongozi wa Chama cha Mouvement Lumumbuste Progressiste aliyemwakilisha Moise Katumbi, Mgombea Urais wa Chama cha Ensemble pour la République. Rais Mstaafu Kikwete pia aliweza kuzungumza kwa simu na Mgombea huyo Mkuu wa Upinzani, Moise Katumbi pamoja na Rais Mstaafu Joseph Kabila.
Mbali na viongozi hao wa Kongo, Dkt Kikwete alikutana na kuzungumza pia na Bintu Keita, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Kongo ambaye pia ni Mkuu wa Majeshi ya Umoja wa Mataifa nchini humo (MONUSCO).
Kiongozi huyo wa POE alitumia fursa ya kuzungumza na wadau hao kuwasihi kushiriki mchakato huo wa uchaguzi kwa amani na kutumia ushawishi wao kuwataka wafuasi wao kutunza amani hususan katika kipindi hiki cha uchaguzi na hata baada ya uchaguzi kumalizika kwa manufaa ya Wanakongo, nchi yao na ukanda mzima.
Aidha, kama sehemu ya misheni hiyo, Jopo hilo la POE lilipata fursa ya kutembelea vituo kadhaa vilivyopo katika jiji la Kishasa na kushuhudia zoezi la upigaji kura lilivyofanyika.
Rais Mstaafu Kikwete anatarajia kukutana na Kiongozi wa Jopo la Wazee wa Busara la Umoja wa Afrika (AU Panel of the Wise) Domitien Ndayizeye, Rais Mstaafu wa Burundi ambapo pamoja na mambo mengine Viongozi hao wawili waliopo nchini DRC wanatarajiwa kujadili na kubadilishana mawazo kuhusu uchaguzi huo kabla ya kuzishauri mamlaka husika za AU na SADC.