Jiji kuu la Ivory Coast, Abidjan kupiga marufuku ombaomba ili kupambana na fujo za mjini

Jiji kuu la Ivory Coast, Abidjan limetangaza kupiga marufuku ombaomba ili kupambana na "fujo za mjini".

"Ili kupambana na fujo za mijini, biashara za kutembea kwenye barabara kuu, kuombaomba kwa namna zote, na matumizi ya mikokoteni sasa yamepigwa marufuku rasmi katika wilaya nzima," alisema naibu gavana Vincent N'cho Kouaoh katika taarifa kwa AFP siku ya Alhamisi.

"Hatua hii inalenga kuboresha hali ya maisha ya watu, kuhakikisha usalama wa watu na mali, na kuboresha ufanisi wa polisi na kazi zao," alisema.

Mwanzoni mwa Machi, gavana wa Abidjan, Ibrahim Cisse Bacongo, alisema "anachukia vitu fulani" kama "wafanyabiashara wa kutembea" na "ombaomba" na alitaka "kupata njia mbadala".

Mwaka 2013, Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamed Bakayoko, alipiga marufuku kuombaomba kwenye makutano ya barabara lakini alishindwa kudhibiti tukio hilo.

Marufuku ya hivi karibuni imekuja baada ya kuondolewa kwa wingi wa ombaomba wa maeneo hatarishi na mitaa ya mabanda huko Abidjan.

Kulingana na Taasisi ya Taifa ya Takwimu, idadi ya watu wa Abidjan iliongezeka kutoka milioni tatu hadi milioni sita kati ya mwaka 1998 na 2021.







Share: