Jeshi la israel latibua shambulizi la hamas baharini

Jeshi la Israel limesema wapiganaji wa kundi la Hamas katika Ukanda wa Gaza walijaribu kujipenyeza na kuingia Israel kupitia baharini.

 Vikosi vya wanamaji viligundua wapiga mbizi waliotumwa na kundi hilo linalotambuliwa kuwa la kigaidi nchini Ujerumani, Marekani na Umoja wa Ulaya, na kulizima shambulizi lao. Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi la Israel wapigambizi wa Hamas walikuwa wamepanga kuvuka upande wa kaskazini kupitia pwani hadi katika kijiji cha mpakani cha Zikim kibbutz, na kwa sasa vikosi vya jeshi vinafanya msako katika eneo hilo.

Vyombo vya habari vya Israel vimesema milio ya risasi imesikika na wanamgambo kadhaa wameuwawa. Jeshi la Israel limesema limeushambulia uwanja wa kijeshi katika Ukanda wa Gaza ambao wanamgambo walikuwa wameutayarisha.

Wakati haya yakiarifiwa katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito mapigano yasitishwe mara moja Gaza. Guterres ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa mashambulizi dhidi ya Gaza yanakiuka sheria ya kimataifa. Balozi wa Israel katika Umoja wa Mataifa Gilad Erdan amejibu kauli hiyo kwa kumtaka Guterres ajiuzulu, akimtuhumu kwa kuonyesha kuelewa na kukubaliana na ugaidi na mauaji katika mashambulizi ya Hamas mnamo Oktoba 7.

Katika matamshi aliyoyatoa kwa Baraza la Usalama jana Jumanne, Guterres alikosoa ukiukaji wa wazi wa sheria ya kimataifa unaoshuhudiwa Gaza. Alisema Wapalestina wamekabiliwa na ukaliaji wa miongo kadhaa, kabla kuongeza kwamba ni muhimu kutambua mashambulizi yaliyofanywa na Hamas hayakufanyika katika ombwe.

Erdan aliandika katika ukurasa wake kwenye mtandao wa X, zamani Twitter na akasema kauli za Guterres zina maana hafai kuuongoza Umoja wa Mataifa.

Share: