Jeff Bezos akanusha taarifa za yeye kufunga ndoa ya kifahari

Mfanyabiashara tajiri namba 2 duniani, Jeff Bezos amekanusha madai kuwa anapanga kufunga ndoa na mchumba wake, Lauren Sánchez, kwa sherehe ya kifahari yenye gharama ya dola milioni 600 huko Aspen, Colorado.

Kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X Jumapili, Bezos alisema, "Hakuna ukweli wowote kuhusu hili, hakuna kitu kama hicho kinachotokea." Aliongeza kuwa uvumi wa uongo husambaa kwa kasi kubwa kuliko ukweli.



Taarifa hii imekuja siku moja baada ya Daily Mail kuripoti kwamba wanandoa hao, waliopanga kufunga ndoa mwishoni mwa Disemba 2024, walikuwa wamekodisha sehemu mbalimbali za kifahari, ikiwa ni pamoja na mgahawa maarufu wa Matsuhisa na shamba la Kevin Costner lenye ukubwa wa ekari 160 kwa ajili ya sherehe hizo.

Bezos, mwenye umri wa miaka 60, na Sánchez, 55, walichumbiana Mei 2023 baada ya miaka mitano ya uhusiano wa kimapenzi. Walianza kuonekana hadharani pamoja mwaka 2019 baada ya talaka ya Jeff Bezos na MacKenzie Scott kukamilika.

Pia, Bezos alimvisha Sánchez pete ya almasi yenye thamani ya dola milioni 2.5, jambo lililothibitishwa na wataalamu wa vito.

Bezos amewatahadharisha watu wake (mashabiki na wafuasi) kutoamini kila kitu wanachosoma mtandaoni.

Share: