Ni jambo la busara kuzingatia kwamba kuna sheria ya kawaida ya kimataifa ambayo haitambui kinga ya serikali kwa kitendo kisicho halali
Mahakama ya Korea Kusini imeiamuru Japan kulipa fidia kundi la wanawake waliolazimishwa kufanya kazi katika madanguro ya kijeshi wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.
Wanawake 16, ambao waliwekwa kama watumwa wa ngono wa wanajeshi wa Japani, kesi yao ilitupiliwa mbali.
Waliwasilisha kesi mwaka wa 2016 lakini Mahakama ya Wilaya ya Seoul iliitupilia mbali miaka mitano baadaye, ikitoa mfano wa kinga ya uhuru.
Hata hivyo, mahakama kuu ya Seoul sasa imebatilisha uamuzi huo.
Katika taarifa mahakama hiyo ilisema inatambua mamlaka ya Korea Kusini juu ya serikali ya Japan kwa sababu wanawake hao waliishi nchini humo na walitaka kulipwa fidia kwa vitendo vilivyoonekana kuwa "haramu".
"Ni jambo la busara kuzingatia kwamba kuna sheria ya kawaida ya kimataifa ambayo haitambui kinga ya serikali kwa kitendo kisicho halali... bila kujali kama kitendo hicho kilikuwa cha uhuru".
Lee Yong-soo, mwanaharakati na mwathiriwa mwenye umri wa miaka 95 alikuwa na hisia kali alipoishukuru mahakama kwa uamuzi huo.
Alipokuwa akiondoka mahakamani aliwaambia waandishi wa habari "Ninashukuru. Ninashukuru sana".
Aliongeza kuwa anatamani angewaambia waathiriwa wote ambao tayari walikuwa wameaga dunia kuhusu hukumu hiyo.
Inakadiriwa kuwa zaidi ya wanawake na wasichana 200,000 walilazimishwa kufanya ukahaba ili kuwahudumia wanajeshi wa Japan katika Vita vya Pili vya Dunia.