Jakaya mrisho kikwete: mzee mwinyi nilimfahamu vizuri mwaka 1984 wakati wa machafuko ya kisiasa.

Mimi nilimfahamu mzee Mwinyi wakati akiwa waziri. Nilikuwa namsoma, namsikiliza kwenye taarifa za habari, baadae akajiuzulu, akawa balozi, akarudi, akawa waziri kwenye ofisi ya makamu wa Rais.

Nilimfahamu kama mtu ambaye ni low profile, hakuwa mtu ambaye anapenda kujipeleka kimbelembele, kuonekana sana

Nilimfahamu vizuri zaidi mwaka 1984 wakati ule wa machafuko ya hali ya kisiasa.

"Kulikuwa na mkutano wa halmashauri kuu ya taifa na mimi nilikuwa mjumbe wa halmashauri kuu ya taifa na ndiyo nimeingia na miaka miwili tu.

Tulipofika pale wajumbe wote tukapangiwa kukaa kwenye hosteli za wanafunzi wa chuo cha biashara, si kawaida, maana tunapewa posho yetu wote tunaenda kutafuta mahali pa kulala.

Tukaanza kuona na baadae tukaja kusimuliwa kwanini lakini mawaziri na wale viongozi wenyeji wa Dodoma walikuwa wanakaa majumbani kwao.

Ila tulikuwa na waziri mmoja tu aliyekuja kukaa na sisi pale hosteli CBE na waziri huyo ni Ali Hassan Mwinyi.

Tukawa tunafanya udadisi kwanini? tukaja kujifunza kwamba ile nyumba aliyopangiwa kukaa waziri mwenzake aliamua kumuweka mtu mwingine" 

Mzee Mwinyi akafika pale anajua hiki ndicho chumba changu cha siku zote akakuta kuna mgeni mwingine akaamua kutokugombana na akaondoka kuja kuungana na sisi pale CBE wajumbe wa kawaida wa NEC.

Lakini tulipokaa nae pale alitupa mapenzi makubwa, hakuwa anadai matunzo tofauti na sisi wengine maana wakati ule mimi nilikuwa jeshini kule Monduli ni meja mkufunzi lakini wakati ule tunaruhusiwa kwenye shughuli za kisiasa na rafiki yangu ambaye tulikuwa tunashea nae chumba alikuwa marehemu kepteni Ditopile Mzuzuri.

Tulikuwa tunakula wote na tulijifunza kuwa ni mtu asiyependa makuu, ni mtu anayeishi katika maisha ya kawaida kama wengine na ana mapenzi kwa watu.

Baada ya mzee Jumbe kujiuzulu,mzee Mwinyi kupendekezwa na mpendekezaji alikuwa Shekh Thabit Kombo, sisi tuliokaa nae pale hosteli tukafurahi sana kwamba ni mtu tunaemfahamu tayari.

Ni mtu muungwana na kwa nafasi ile Zanzibar watakuwa wamepata kiongozi thabiti.

"Watu wanasema kila kitu kinatokea kwasababu yake, pengine yule aliyemkataa mwanzo labda Mwenyenzi Mungu alimuongoza mzee Mwinyi aje akae na sisi pale ili wajumbe wengi wa NEC tumfahamu kwa hilo ambalo lingekuja kutokea mbele yake."

Funzo la kwanza ni hilo usihamanike mambo yanapotokea, kuwa mvumilivu, mstahamilivu, huenda kuna sababu Mungu anayafanya hayo yatokee.

Mara ya pili kumfahamu mzee Mwinyi ni pale aliponiteua kuwa Mbunge na naibu waziri wa nishati na madini.

"Nilipokwenda kumuona kwanza nilimuambia hii ya ubunge nzuri ila hii ya unaibu waziri siijui maana sijawahi kufanya kazi serikalini,akaniambia wewe ni kijana,mahiri na unaweza, kila la kheri.

"Nilichojifunza kingine alikuwa ni mtu mwenye kuamua, alikuwa hana uoga kwenye kuamua. Unamuona ni mtu mpole,rahimu lakini jambo aliloliamini kwamba hili ni sawa na lina maslahi kwa taifa ataamua."

Yeye tumkumbuke kama baba wa mageuzi.Mageuzi ya kiuchumi na ya kisiasa.Haikuwa rahisi.

Namshukuru Mzee Mwinyi, binafsi aliponiteua kuwa naibu waziri ndiye aliyenianzishia safari yangu iliyokuja hatimaye kuwa Rais wa nchi yangu.

Kama nilivyosema nilikuwa kwenye jeshi na matumaini yangu yalikuwa kuishia huko na kwenye chama.Alichokiona kwangu sijui lakini nimefika nilipofikia, namshukuru sana.

Jakaya Mrisho Kikwete Rais Mstaafu wa Tanzania

Share: