Mzee Mwinyi baada ya Rais wa Zanzibar kujiuzulu, alipewa mzigo wa kwenda kuituliza Zanzibar
"Leo ni siku ya majonzi makubwa kwa kuondokewa na Mzee Mwinyi lakini pia ni siku ya kusherehekea maisha yake.
Mzee Mwinyi alilitumikia taifa hili kwa muda mrefu na alilisaidia taifa katika juhudi zake za kuleta maendeleo.
Mzee Mwinyi aliposhika uongozi wa nchi hii tulikuwa na matatizo makubwa kwa upande wa uchumi na kisiasa.
Kabla ya kushika uongozi huko nyuma yalikuwa yametokea matukio ambayo yaliathiri juhudi zetu za maendeleo. Kuvunjika kwa jumuiya ya Afrika mashariki, vita vya Uganda, kupanda kwa bei ya mafuta; kulifanya uchumi wetu ukadorora."
Na aliposhika uongozi hali ilivyokuwa wakati huo, ilikuwa ni mbaya sana.
Sasa hivi tuna matatizo, tuna upungufu wa sukari, tuna matatizo ya umeme, tuna tatizo la maji lakini matatizo tuliyonayo sasa hivi ni madogo sana ukilinganisha na wakati wa Mzee Mwinyi.
Alikuta nchi ina upungufu wa mafuta na shughuli za kiuchumi, kijamii zilikuwa zinakwama. Alikuta nchi haina bidhaa adimu madukani.
Alikuta nchi ina upungufu wa chakula na katika mazingira ambayo hatukuwa na rasilimali za kutosha, mzee Mwinyi aliunda timu ya kumsaidia ili kupambana na matatizo ya uchumi.
"Mimi nilikuwa mmojawapo katika timu hiyo kama msaidizi wake namba moja na kwa kipindi kama cha miaka mitatu tulifanya kazi usiku na mchana.
Matunda yake chini ya uongozi wake baada ya miaka mitatu, hali ya mafuta ilitengamaa. Bidhaa zilianza kupatikana ikiwa ni matokeo ya RHUKSA na njaa wananchi walikuwa wamelima na baada ya miaka mitatu tatizo letu halikuwa upungufu wa chakula, tatizo letu lilikuwa upungufu wa hifadhi.
Baada ya miaka mitano Mzee Mwinyi alikuwa ameliongoza taifa likatulia na tukaanza safari ya maendeleo. Kulikuwa pia na matatizo ya kisiasa, wote mtakumbuka mwaka 1984 tulikuwa na matatizo Zanzibar.
Mzee Mwinyi baada ya Rais wa Zanzibar kujiuzulu, alipewa mzigo wa kwenda kuituliza Zanzibar na kwa miaka miwili aliituliza Zanzibar.
Matatizo ya kisiasa bado yalikuwepo kwa nchi nzima, mtakumbuka 1988 kulikuwa na mpasuko wa uongozi katika nchi yetu hata baadhi ya viongozi wakajiondoa kwenye chama.
Ni wakati huohuo kulikuwa na vuguvugu la kuleta mabadiliko ya kisiasa dunia nzima. Mzee Mwinyi aliunda tume ya Nyalali ikaleta mapendekezo.
Haikuwa rahisi kufikia uamuzi wa mabadiliko ya aina gani, lakini chini ya uongozi wake maamuzi yalifanywa. Wakati wote ule mageuzi yalikuwa yanafanywa kwa kuzingatia kwamba tusije tukahatarisha umoja wetu, mshikamano wetu. Mzee Mwinyi aliwekea mkazo kwenye hilo."
".... Mabadiliko makubwa yalifanywa lakini nchi ikabaki imetulia."
Mzee Joseph Sinde Warioba Jaji na Waziri mkuu mstaafu.