Israel yashambulia maeneo 250 ya ukanda wa gaza kwa siku

Jeshi la Israel limesema mapema leo kwamba vikosi vyake vimeyashambulia zaidi ya maeneo 250 katika Ukanda wa Gaza ndani ya siku moja.

Limeongeza kuwa vikosi vyake vilifanya mashambulizi ya umakini kutoka angani, baharini na ardhini dhidi ya ngome za "magaidi" jana Jumanne.

Kulingana na Israel, wanamgambo wa Kipalestina pia walirusha makombora kuelekea Israel  katika miji ya mpakani karibu na Ukanda wa Gaza.

Jeshi la Israel pia lilitangaza vifo vya wanajeshi wake 10 waliouawa Jumanne. Jumla ya wanajeshi 115 wa Israel wameuawa tangu ilipoanzisha operesheni yake ya ardhini dhidi ya Hamas, kundi ambalo Marekani, Umoja wa Ulaya na nchi nyingine hulichukulia kuwa la kigaidi.

Kulingana na wizara ya Afya ya Gaza inayodhibitiwa na Hamas, idadi ya Wapalestina waliouawa tangu vita hivyo vilipoanza Oktoba 7, imepita 18,400.

Share: