ISRAEL YAMUUA MSEMAJI WA HAMAS, ABU OBEIDA

Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, alitangaza Jumapili kwamba msemaji wa Hamas, Abu Obeida, ameuawa Gaza mwishoni mwa wiki.

Taarifa ya mwisho ya Abu Obeida ilitolewa Ijumaa, wakati Israel ilipoanza hatua za awali za mashambulizi mapya ya kijeshi katika Jiji la Gaza, na kulitangaza eneo hilo kuwa la mapigano. Hamas haijatoa maoni yoyote kuhusu madai ya Israel.

Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu awali alisema kuwa Israel ilimshambulia Obeida, msemaji wa muda mrefu wa Brigedi za Qassam za Hamas, lakini hakujua kama aliuawa au la.

“Naona hakuna mtu upande wa Hamas anayejiuliza swali hili,” Netanyahu aliwaambia mawaziri katika kikao cha baraza la mawaziri la kila wiki.

Obeida ndiye mwakilishi wa hivi karibuni wa Hamas kulengwa na kuuawa na Israel katika jitihada za kudhoofisha uwezo wa kijeshi wa kundi hilo.

Tangu Jumamosi, Wapalestina wasiopungua 43 wameuawa, wengi wao katika Jiji la Gaza, kwa mujibu wa hospitali za eneo hilo. Hospitali ya Shifa — kubwa zaidi katika eneo hilo — ilisema miili 29 imeletwa mochari, wakiwemo watu 10 waliouawa wakitafuta msaada na wengine waliouawa katika maeneo mbalimbali ya jiji.

Asubuhi ya Jumapili, maofisa wa hospitali waliripoti vifo vingine 11 kutokana na mashambulizi na risasi. Hospitali ya Al-Awda ilisema saba kati ya hao walikuwa raia waliokuwa wakijaribu kufuata misaada.

Mashahidi walisema wanajeshi wa Israel walifyatua risasi kwa umati katika Korridori ya Netzarim, eneo la kijeshi la Israel linalogawanya Gaza.

Share: