Wanajeshi pia wameripotiwa kuingia ndani zaidi katika maeneo yaliyosalia ya mji, ambapo wanaamini kuwa viongozi wa Hamas wamejificha kwenye mahandaki na mateka.
Jeshi la Israel linasema kuwa vikosi vyake vya ardhini vimezingira mji wa Khan Younis, ambao ndio mkubwa zaidi kusini mwa Ukanda wa Gaza.
Wanajeshi pia wameripotiwa kuingia ndani zaidi katika maeneo yaliyosalia ya mji, ambapo wanaamini kuwa viongozi wa Hamas wamejificha kwenye mahandaki na mateka.
Wakaazi walisema kuwa vifaru vilifunga barabara ya mwisho kutoka nje ya jiji kuelekea pwani ya Mediterania, na kuwazuia kukimbilia kusini.
Pia kulikuwa na mapigano makali karibu na hospitali kuu mbili za jiji hilo.
Makabiliano haya yanajiri wakati mazishi yakifanyika kwa baadhi ya wanajeshi 24 wa Israel waliouawa siku ya Jumatatu katika siku mbaya zaidi kwa Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) tangu kuanza kwa mashambulizi yake ya ardhini huko Gaza wiki 12 zilizopita.
Takriban Wapalestina 195 pia waliuawa huko Gaza katika muda wa saa 24 zilizopita, kulingana na wizara ya afya ya eneo hilo inayoendeshwa na Hamas.
Wizara hiyo inasema zaidi ya watu 25,400 wameuawa - wengi wao wakiwa watoto na wanawake - wakati wa vita kati ya Hamas na Israel.
Vita hivyo vilichochewa na shambulio la kuvuka mpaka ambalo halijawahi kufanywa na wapiganaji wa Hamas kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba, ambapo takriban watu 1,300 waliuawa - wengi wao wakiwa raia - na wengine wapatao 250 walichukuliwa mateka.