Iran yakanusha kuhusika na shambulizi la ndege zisizo na rubani lililouwa wanajeshi wa marekani

Ni mara ya kwanza kwa shambulio kuua wanajeshi wa Marekani katika eneo hilo tangu shambulizi la Hamas la tarehe 7 Oktoba dhidi ya Israel.

Iran imekanusha kuhusika na shambulio la ndege isiyo na rubani kwenye kituo cha kijeshi cha Marekani karibu na mpaka wa Jordan na Syria na kusababisha vifo vya wanajeshi watatu wa Marekani.

Marekani ililaumu shambulio hilo dhidi ya "makundi ya wapiganaji wenye itikadi kali wanaoungwa mkono na Iran" ambayo pia yamesababisha makumi ya watu kujeruhiwa.

Rais wa Marekani Biden aliapa kulipiza kisasi na kusema: "Tutajibu."

Ni mara ya kwanza kwa shambulio kuua wanajeshi wa Marekani katika eneo hilo tangu shambulizi la Hamas la tarehe 7 Oktoba dhidi ya Israel.

Kumekuwa na mashambulizi mengine kwenye kambi za Marekani katika eneo hilo, lakini kabla ya Jumapili hakukuwa na vifo vilivyoripotiwa kutokea, kulingana na jeshi la Marekani.

Haijabainika ni nani aliye nyuma ya shambulio hili la hivi punde.

Bw Biden alisema Marekani "itawawajibisha wale wote waliohusika kwa wakati na kwa njia tunayochagua".

Iran ilikanusha shutuma za Marekani na Uingereza kwamba inaunga mkono makundi ya wanamgambo wanaolaumiwa kwa shambulizi hilo.

"Madai haya yanatolewa kwa malengo mahususi ya kisiasa ili kubadili hali halisi ya eneo," msemaji wa wizara ya mambo ya nje Nasser Kanaani alisema, kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la IRNA la Tehran.

Ikulu ya White House ilisema Bw Biden aliarifiwa Jumapili asubuhi juu ya shambulio hilo na Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin na maafisa wengine.

Share: