Iran:  anyongwa kwa kosa la kumuua mumewe na kutumikia miaka 10 jela

Samira Sezian raia wa Iran mwenye umri wa miaka 30, aliyefungwa kwa kumuua mumewe, amenyongwa baada ya kutumikia kifungo cha miaka 10 jela.

Alinyongwa katika gereza la Ghezel Hesar katika mji wa Karaji, Tehran, kwa mujibu wa kundi la Haki za Kibinadamu la Iran (IHR) lenye makao yake Norway.

Kunyongwa kwake kunakuja huku wasiwasi ukiongezeka juu ya idadi ya watu walionyongwa nchini Iran mwaka huu, huku mamia ya watu wakihukumiwa kunyongwa hasa kwa makosa ya dawa za kulevya na mauaji .

Wizara ya Sheria ilisema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kwamba Samira alimuua mumewe kwa makusudi kwa kuchanganya sumu katika vinywaji vyake.

Kulingana na ripoti ya shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, Samira aliolewa akiwa na umri mdogo. Nayo ripoti ya Human Rights Watch Foundation, inasema mahakama ilimshtaki kwa kumuua mumewe Januari 2014.

Wakati huo, Samira alikuwa na umri wa miaka 19 na alimuua mumewe kwa msaada wa mdogo wake wa kike aliyekuwa na umri wa miaka 14 na mtu mwingine.

Mahakama ilisema katika taarifa kwa vyombo vya habari, "familia ya marehemu ilishikilia hukumu ifanyike na pande hizo mbili zilishindwa kufikia muafaka, uamuzi huu umetolewa baada ya jitihada nyingi."

Katika taarifa hiyo imeelezwa sababu ya kuchelewa kwa hukumu: "Uamuzi huo ulicheleweshwa sana kwa sababu tulikuwa tunajaribu kupatanisha kati ya familia za pande zinazohusika."

Aliletwa katika gereza la Varamin katika jiji la Karchak ili kusikiliza uamuzi wa mahakama. Vyombo vya habari vya Iran viliripoti: "Samira alikosa la kusema baada ya uamuzi."

Ripoti hiyo inaongeza: "Aliporudishwa gerezani, hakuweza kutembea na alirudishwa akiwa kwenye kiti cha magurudumu."

Amnesty International inasema "imeshtushwa" na ripoti za "unyongaji huo wa kutisha."

Nayo Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa inasema, imesikitishwa na mauaji hayo, ''tunaitaka tena Iran kusitisha kutoa hukumu ya kifo.''

Kwa mujibu wa ripoti kutoka Iran, Samira alikamatwa baada ya mtu mmoja aitwaye Nima kuuawa katika nyumba moja katika jiji la Karaj Januari 15, 2014.

Samira aliolewa akiwa mdogo na alipata watoto wawili wenye umri wa miaka 11 na 15 sasa.

Mwanaharakati wa haki za binadamu Xila Mustajr anasema, ''Samira alihukumiwa kifo katika mahakama isiyo ya haki na isiyo na uwazi, ambapo alikuwa chini ya shinikizo na kukiri kosa.''

Mwanaharakati huyo wa haki za binadamu pia anasema, "mbali na juhudi za mashirika ya haki za binadamu na taasisi za kimataifa, serikali ya Iran ilichukua uamuzi wa kuchukua maisha yake. Samira pia alikuwa mhanga wa unyanyasaji wa nyumbani na ndoa ya utotoni. Ni mwathirika wa sheria za chuki dhidi ya wanawake."

Vyombo vya habari vya ndani nchini Iran viliripoti - familia ya marehemu ilisisitiza kuwa amri ya mahakama hiyo itekelezwe haraka iwezekanavyo.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yameibua wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa mauaji nchini Iran mwaka huu, huku takriban watu 115 wakiuawa mwezi Novemba pekee kulingana na Amnesty International.

Kwa mujibu wa IHR, wanawake 18 sasa wamenyongwa nchini Iran mwaka huu, akiwemo Samira. Iran iliwanyonga watu 582 mwaka 2022 lakini mwaka huu idadi inatarajiwa kuwa kubwa zaidi.

Share: