INDONESIA YAPUNGUZA MARUPURUPU YA WABUNGE KUFUATIA MAANDAMANO

Rais wa Indonesia, Prabowo Subianto, ametangaza kupunguzwa kwa marupurupu ya wabunge baada ya maandamano ya kupinga serikali kusababisha vifo vya angalau watu watano — vurugu mbaya zaidi nchini humo katika miongo kadhaa.

Maandamano yalianza Jumatatu wiki iliyopita wakazi na wanafunzi wakipinga kile walichokiita posho kubwa na malipo ya makazi kwa wabunge. Hali iligeuka kuwa ghasia Ijumaa baada ya dereva wa bodaboda wa huduma za mtandaoni kuuawa wakati polisi walipokuwa wakitawanya waandamanaji.

Wakati ghasia zikiendelea, nyumba za viongozi wa vyama vya siasa na majengo ya serikali yalivamiwa au kuchomwa moto, hali iliyoyumbisha imani ya wawekezaji na kusababisha kushuka kwa thamani ya hisa na sarafu ya Indonesia. Miongoni mwa walilengwa ni Waziri wa Fedha Sri Mulyani Indrawati, ambaye nyumba yake ilivunjwa usiku wa kuamkia Jumapili nje ya mji mkuu Jakarta.


Akizungumza Ikulu akiwa ameambatana na viongozi wa vyama vya siasa, Rais Prabowo alisema bunge limekubali kufuta sera kadhaa ikiwemo kupunguza posho za wabunge na kusitisha safari zao za kikazi nje ya nchi. Wakati huohuo, aliagiza jeshi na polisi kuchukua hatua kali dhidi ya waharibifu, wavamizi na waporaji, akiongeza kuwa baadhi ya matukio yanaashiria vitendo vya “ugaidi na uhaini.”


Hata hivyo, mashirika ya wanafunzi na makundi ya haki za binadamu yamekosoa hatua hizo. Muzammil Ihsan, kiongozi wa umoja mkubwa wa wanafunzi nchini humo, alisema kupunguza marupurupu pekee hakutoshi kwani hasira za wananchi zinatokana na matatizo makubwa zaidi ya kiuchumi na kisiasa. Tegar Afriansyah, kiongozi wa kundi jingine la wanafunzi, alitaja agizo la Rais kwa jeshi na polisi kuwa ni “ukandamizaji na vitisho.”

Amnesty International Indonesia pia lilikosoa matumizi ya maneno kama “uhaini” na “ugaidi,” likiita ni kupita kiasi.

Taarifa za Jumapili zilionyesha idadi ya waliokufa kufikia watano, wakiwemo watu watatu waliouawa katika shambulio la moto kwenye jengo la bunge la jimbo na dereva wa bodaboda aliyeuawa na umati uliomtuhumu kuwa jasusi.

Kwa sasa, maandamano mapya yamepangwa kufanyika Jumatatu huku Prabowo akiahirisha ziara yake ya China kushughulikia hali ya usalama. Jeshi limepelekwa kulinda Ikulu na nyumba za mawaziri, ishara ya jinsi hali ya sintofahamu ilivyozidi.

Share: