Hisa za kampuni ya Nissan zaongezeka kwa kiwango kikubwa wakati Honda zikishuka
Hisa za Nissan Motor zilipanda kwa kiwango kikubwa Jumatano kufuatia ripoti ya vyombo vya habari kwamba mtengenezaji magari huyo wa Kijapani anayekabiliwa na changamoto anapanga kuungana na Honda Motor ili kuunda taasisi kubwa zaidi inayoweza kushindana na wapinzani wakubwa na kuwekeza zaidi kwenye soko linalokua la magari ya umeme.
Kwa mujibu wa ripoti ya gazeti la Nikkei, Honda na Nissan wanazingatia kufanya kazi chini ya kampuni mama, huku wakipanga kusaini hati ya makubaliano hivi karibuni. Wanatarajia pia kuingiza Mitsubishi Motors, ambapo Nissan inamiliki asilimia 24 ya hisa, chini ya kampuni hiyo mama.
Hisa za Nissan ziliongezeka kwa asilimia 23.7, ikiwa ni siku bora zaidi kwa kampuni hiyo tangu mwaka 1985, kwa mujibu wa data kutoka Factset, huku hisa za Honda zikishuka kwa asilimia 3.