suala la rushwa, naomba niwe wazi, sitalivumilia, tutalifanyia kazi, haiwezekani viongozi watueleze suala hili mara kwa mara
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Dkt. James Andilile, amewataka wafanyakazi wa Mamlaka hiyo kutekeleza wajibu wao kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo ili kuleta tija na ufanisi katika majukumu yao ya kila siku.
Dkt. Andilile ameyasema wakati akiahirisha kikao cha kwanza cha mkutano wa pili wa Baraza la Wafanyakazi wa EWURA, kilichofanyika jijini Dodoma kwa siku mbili kuanzia 8 Novemba 2023.
“ Niwakumbushe wafanyakazi wenzangu, tudai haki zetu lakini tusisahau kuwa pia tunao wajibu juu ya haki hizo, ninawasisitiza kulizingatia suala hilo kwani sote tunafahamu hakuna haki bila wajibu”. Alisema Dkt Andilile.
Mkurugenzi Mkuu huyo, pia, amewasisitiza wafanyakazi kuwahi kazini, kuwa wamoja na kujiepusha na vitendo vya rushwa na kutekeleza majukumu waliyopangiwa kwa ufasaha bila kusukumwa, na kuwa kwa kufanya hivyo ni kuchochea uimara wa taasisi.
“Kwenye suala la rushwa, naomba niwe wazi, sitalivumilia, tutalifanyia kazi, haiwezekani viongozi watueleze suala hili mara kwa mara, wao wana taarifa nyingi, tujiangalie, lisemwalo lipo kama halipo laja” Alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Dkt. Andille amewaelekeza Wakuu wa Idara, Vitengo na Kanda kuwasimamia wafanyakazi katika maeneo yao ili kuhakikisha kuwa kila mmoja anatekeleza majukumu aliyopangiwa kwa wakati na kwa ufanisi.