Haiti imetangaza hali ya tahadhari ya saa 72 na amri ya kutotoka nje usiku

Haiti imetangaza hali ya tahadhari ya saa 72 na amri ya kutotoka nje usiku ndani na karibu na mji mkuu kwa sababu ya kuvamiwa kwa magereza mawili na ukosefu wa usalama unaoendelea.

Mwishoni mwa juma, magenge yenye silaha yalivamia gereza kubwa la Port-au-Prince, na kusababisha mauaji ya takriban watu 12 na kuachiliwa kwa karibu wafungwa 4,000.

Viongozi wa magenge wanasema wanataka kumlazimisha Waziri Mkuu Ariel Henry, ambaye yuko nje ya nchi ajiuzulu.

Idadi kubwa ya wanaume wapatao 4,000 waliokuwa wameshikiliwa humo sasa wametoroka, mwandishi wa habari wa eneo hilo alisema.

Miongoni mwa waliozuiliwa ni wanachama wa genge walioshtakiwa kuhusiana na mauaji ya mwaka 2021 ya Rais Jovenel Moïse.

Ghasia nchini Haiti, ambayo ni nchi maskini zaidi katika bara la Amerika, zimezidi kuwa mbaya katika miaka ya hivi karibuni. Magenge yanayolenga kumtimua Waziri Mkuu Ariel Henry yanadhibiti 80% jiji la Port-Prince.


Ongezeko la hivi punde la ghasia lilianza Alhamisi, wakati waziri mkuu aliposafiri hadi Nairobi kujadili kutuma kikosi cha usalama cha kimataifa kinachoongozwa na Kenya nchini Haiti.

Kiongozi wa genge Jimmy Chérizier (jina la utani "Barbeque") alitangaza shambulio lililoratibiwa lililolenga kumuondoa.

"Sisi sote, makundi yenye silaha katika miji ya mkoa na makundi yenye silaha katika mji mkuu, tumeungana," alisema afisa huyo wa zamani wa polisi, ambaye anadhaniwa kuhusika na mauaji kadhaa katika Port-au-Prince.

Wimbi la risasi lilisababisha vifo vya maafisa wanne wa polisi na watano kujeruhiwa. Ubalozi wa Ufaransa nchini Haiti ulishauri dhidi ya kusafiri ndani na kuzunguka mji mkuu.

Muungano wa polisi wa Haiti uliuliza wanajeshi kusaidia kuimarisha gereza hilo, lakini boma lilivamiwa Jumamosi jioni.

Siku ya Jumapili milango ya gereza hilo ilikuwa bado wazi na hakukuwa na dalili zozote za maafisa, shirika la habari la Reuters liliripoti. Wafungwa watatu waliojaribu kutoroka walikuwa wamekufa, ripoti hiyo ilisema.

Share: