Gilead terry: serikali ya awamu ya sita imetoa misamaha mingi ya kodi na kuweka vivutio vingi vya uwekezaji kwenye sekta ya utalii

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji nchini Tanzania Bwana Gilead Terry amesema Serikali ya awamu ya sita imetoa misamaha mingi ya kodi na kuweka vivutio vingi vya uwekezaji ili kuvutia zaidi watanzania na wageni wengi zaidi kuwekeza kwenye sekta ya Utalii.

Terry ameyasema hayo wakati akizungumza na wanahabari nje ya Ukumbi wa mikutano Grand Melia kabla ya kuanza kwa kongamano la uwekezaji kwenye sekta ya Utalii Mkoani Arusha.

Terry amewaambia wanahabari kuwa lengo la kongamano hilo ni kuwajulisha wadau wa sekta ya utalii kuhusu fursa hizo za utalii na nafuu mbalimbali zilizowekwa na serikali kupitia sheria ya Uwekezaji ya mwaka 2022.

Kongamano hilo pia kulingana na TIC, litakuwa na majadiliano na wadau waliopo kwenye sekta ya Utalii mkoani Arusha ili kujua fursa na changamoto zilizopo ili kuongeza kiwango cha uwekezaji kwenye sekta hiyo.

Kongamano hili linalofanyika leo Aprili 29, 2024 linaongozwa na Waziri wa Nchi, ofisi ya Rais, mipango na uwekezaji Mhe. Profesa Kitila Mkumbo kwa kushirikiana na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Angela Kairuki.

Kongamano hilo linafuatia maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan alilolitoa wakati akiwaapisha viongozi mbalimbali akimtaka Mkuu wa Mkoa wa Arusha kushughulikia changamoto ya upatikanaji wa vyumba vya kulala wageni wanaotembelea Mkoa wa Arusha.

Mwenyeji wa Kongamano hili ni Mheshimiwa Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Arusha.

Share: