Gaza: israel inasema mateka 136 bado wanazuiliwa na hamas

Hamas yasema inachunguza pendekezo la kusitishwa upya kwa mapigano Gaza Kiongozi wa kisiasa wa Hamas amethibitisha kuwa wanachunguza pendekezo jipya la kusitishwa kwa mapigano katika ukanda wa Gaza.

Ismail Haniyeh alisema kuwa kundi hilo limealikwa kujadili mpangokazi wa Israel, Marekani, Qatar na Misri.

Inaripotiwa kuwa zimependekeza kusitishwa mapigano kwa wiki sita, wakati ambapo kutakuwa na mabadilishano ya waliochukuliwa mateka kati ya Israel na Palestina.

Haniyeh alisistiza kipaumbele cha Hamas ilikuwa ni mpango wa kudumu wa kusitisha vita na kujiondoka kabisa kwa Israel, lakini Waziri mkuu wa Israel alifutilia mbali uwezekano huo.

Benjamin Netanyahu alisistiza kuwa mapigano hayataisha hadi watakapopata "ushindi kamili" ambao alisema utamaanisha kumaliza kabisa kundi la Hamas na kuachiliwa huru kwa walioshikwa mateka.

Mzozo huo ulichochewa na shambulio la kuvuka mpaka ambalo halijawahi kushuhudiwa na watu wenye silaha wa Hamas kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba, ambapo takriban watu 1,300 waliuawa na wengine wapatao 250 kuchukuliwa mateka.

Zaidi ya watu 26,700 wameuawa huko Gaza tangu wakati huo, kulingana na wizara ya afya ya eneo hilo inayoendeshwa na Hamas.

Wakati wa usitishaji vita wa wiki nzima mwishoni mwa mwezi Novemba, mateka 105 wa Israel na wa kigeni waliachiliwa kwa kubadilishana na Wapalestina 240 waliokuwa wakishikiliwa katika jela za Israel.

Israel inasema mateka 136 bado wanazuiliwa, ingawa karibu dazeni mbili kati ya hao wanakisiwa kuwa wamekufa.

Share: