Finland nchi ya kwanza ya nordic kujadiliana kidipolomasia na tanzania

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mara ya kwanza imefanya majadiliano ya kidiplomasia na Serikali ya Finland kwa lengo la kuimarisha, kukuza na kudumisha ushirikiano katika sekta mbalimbali za kipaumbele kwa maslahi ya pande zote mbili.

Pamoja na Tanzania kuwa na uhusiano mzuri na nchi za Nordic, Finland ndiyo nchi ya kwanza kufanya majadiliano ya kidiplomasia na Tanzania. Chimbuko la majadaliano hayo ni kuendelea kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na nchi za Umoja wa Ulaya.

Mkutano huo kwa upande wa Tanzania umeongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) wakati upande wa Finland umeongozwa na Naibu Waziri katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Finland anayeshughulikia Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa, Mhe. Pasi Hellman.

Akizungumza katika mkutano uliokutanisha pande hizo mbili Jijini Dar es Salaam, Waziri Makamba amesema kuwa kutetea na kulinda misingi ya demokrasia na utawala bora ni kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Waziri Makamba ameeleza kuwa maboresho yaliyofanyika katika sheria ya vyama vya siasa na sheria ya uchaguzi yameleta mageuzi katika kuendesha chaaguzi mbalimbali nchini na uhuru wa vyama vya siasa kuendesha shughuli zake nchini.

Aidha, Tanzania itaendelea kulinda na kukuza misingi ya haki za binadamu, demokrasia na utawala bora kama nguzo muhimu ya kuleta maendeleo endelevu nchini.

Kwa upande wake, Naibu Waziri katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Finland anayeshughulikia Ushirikiaano wa Maendeleo ya Kimataifa, Mhe. Pasi Hellman amesema ushirikiano kati ya Finland na Tanzania umekuwa imara kwa zaidi ya miaka 50 na utaendelea kuimarika kutokana na misingi imara ya ushirikiano iliyopo baina ya mataifa hayo.

Share: