Esteban lazo hernández atawasili nchini kenya kupata ufafanuzi kuhusu madaktari waliotekwa nyara

Rais wa Bunge la Cuba, Esteban Lazo Hernández, amesafiri nchini Kenya ili kupata ufafanuzi kuhusu ripoti za hivi majuzi ambazo hazijathibitishwa ambazo zilidokeza kuwa madaktari wawili wa Cuba waliotekwa nyara nchini Kenya mwaka 2019 walikuwa wameuawa.

Madaktari hao, Assel Herrera Correa na Landy Rodríguez Hernández, walitekwa nyara na wanamgambo wa al-Shabaab walipokuwa wakisafiri kwenda kazini.

Wikiendi iliyopita, al-Shabaab walisema kwamba madaktari hao waliuawa Alhamisi iliyopita wakati wa shambulio la ndege zisizo na rubani za Marekani zilizolenga nyumba moja katika mji wa Jilib kusini mwa Somalia.

Afisa wa ulinzi wa Marekani alinukuliwa na kituo cha habari cha CNN akisema kwamba hakuna ushahidi wa kuaminika kwamba shambulio hilo lilisababisha vifo vya raia, lakini akaongeza kuwa Marekani ilikuwa inachunguza madai ya al-Shabaab ya vifo vya madaktari.

Wizara ya mashauri ya nchi za kigeni ya Cuba inasema pia imewasiliana na serikali za Marekani na Somalia kwa maelezo zaidi kuhusu operesheni ya kijeshi inayohusishwa na hali ya madaktari hao.

Baada ya utekaji nyara wa 2019, wapiganaji wa al-Shabaab kisha walimuua polisi aliyekuwa na silaha aliyekuwa akiwalinda madaktari.

Kundi hilo la wanamgambo kisha liliwapeleka madaktari hao katika nchi jirani ya Somalia, na baadaye kudai fidia ya dola milioni 1.5 ili madaktari hao waachiliwe.

Share: