
Rais Mteule wa Marekani Donald Trump amesema atafanya mazungumzo na Viongozi wa Ukraine na Urusi kumaliza alichokitaja kuwa umwagaji damu kutokana na vita vya karibu miaka mitatu baina ya Nchi hizo mbili.
Mtandao wa DW Kiswahili umeripoti kuwa Trump amesema hayo wakati akiongea kwa mara ya kwanza na Waandishi wa Habari tangu alipochaguliwa kwa mara nyingine kuwa Rais wa Marekani ambapo amesema ni lazima mauaji yanayotakana na vita hivyo yakomeshwe, akiahidi kwa mara nyingine kuumaliza mzozo huo atakapoingia madarakani.
“Tutazungumza na Rais Putin, na tutazungumza na Wawakilishi wa Zelensky na Wawakilihsi wa Ukraine, ni lazima tukomeshe (vita), ni mauaji yasiyoelezeka”
Trump mara kadhaa amedai kuwa na uwezo wa kumaliza mzozo wa Ukraine haraka lakini hadi sasa hajaweka wazi hadharani mkakati wake wa kufanya hivyo na hivi karibuni alitoa wito wa kushitishwa mara moja kwa mapigano na akasema mazungumzo yanapaswa kuanza haraka.