Dkt.gwajima "wawezesheni maafisa maendeleo ya jamii kushiriki kongamano la wataalamu wa maendeleo ya jamii"

Waziri wa Maendeleo ya Jamii , Jinsia Wanawake na Makundi Maalum Dkt.Dorothy Gwajima ametoa wito kwa waajiri wa Maafisa Maendeleo ya Jamii kwenye Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, Serikali Kuu, Mashirika ya Umma, Taasisi za Elimu, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na Taasisi nyingine zote kuwawezesha wataalamu hao kushiriki kongamano la wataalamu wa Maendeleo ya Jamii 2023.

Kongamano hilo litafanyika Novemba 20- 22, 2023 na litakwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 60 ya chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru kikitarajiwa kushirikisha jumla ya washiriki 1500 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar watashiriki kongamano wakiwemo kutoka; Sekretarieti na Mamlaka za Serikali za Mitaa; Serikali Kuu; Mamlaka mbalimbali za Serikali; Vyuo na Taasisi za elimu ya Juu; Mashirikia yasiyo ya Kiserikali; Mashirika ya kimataifa; Mashirika ya dini; Mabonde ya Maji; Majeshi; Taasisi za kifedha na Sekta binafsi.

Akizungumza na Waandishi wa habari kuelekea Kongamano hilo leo Novemba 6,2023 Jijini Dodoma Dkt.Gwajima amesema ada ya ushiriki shilingi 350,000/=.

Dkt.Gwajima amesema, lengo kuu la kongamano ni kutoa fursa ya wataalamu kujadiliana juu ya mchango wa sekta ya maendeleo ya jamii na changamoto kwenye maendeleo ya taifa pamoja na kuendelea kubuni mbinu za kutekeleza mipango ya Serikali ya awamu ya sita katika kuwezesha wananchi kujiletea maendeleo endelevu kwa kutumia rasilimali zinazowazunguka. Kaulimbiu ya kongamano hili ni “Sekta ya Maendeleo ya Jamii: Msingi Imara wa Uwezeshaji wa Wananchi.”

Share: