Dk. nchimbi amefanya mazungumzo na balozi wa marekani nchini

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel John Nchimbi amesema dhamira ya Mwenyekiti wa CCM ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha Nchi inaongozwa kwa kuzingatia misingi ya demokrasia na utawala bora na hivyo haipaswi kutiliwa shaka hata kidogo.

Balozi Nchimbi amesema katika utekelezaji wa dhana ya utawala bora, chini ya uongozi wa Rais Samia, Tanzania imeendelea kushuhudia kuwapo kwa uhuru wa mihimili mitatu ya dola, ambayo ni Serikali, Bunge na Mahakama.

Amesema mihimili hiyo ya dola imeendelea kutimiza wajibu wake kwa kufanya kazi vizuri na hivyo kuaminiwa na Wananachi, Balozi Nchimbi amesisitiza kuwa CCM chini ya Rais Samia, kitahakikisha dhamira hiyo pia inaendelezwa kwa vitendo kwa kuunga mkono uwapo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar kwa maslahi ya Nchi na Taifa kwani umoja huo ni zaidi ya vyama vya siasa.

Katibu Mkuu huyo wa CCM amesema hayo leo Jumanne, March 5, 2024, alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Marekani nchini, Michael Battle, kwenye Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba, jijini Dar es Salaam, ambapo viongozi hao walijadiliana masuala anuai kuhusu ushirikiano na uhusiano wa muda mrefu kati ya Nchi hizo mbili.

Share: