Chama Cha Mawakili Kanda ya Kaskazini kimesema kimejiandaa vyema katika utoaji wa huduma ya Msaada wa kisheria kwa wananchi wote wa Arusha watakaojitokeza kwenye Programu maalum iliyoandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda.

Akizungumza na Wanahabari mapema leo Mei 07, 2024, Wakili George Steven Njohoka, Mwenyekiti wa Chama Cha Mawakili Kanda ya Arusha amesema Ofisi za Mawakili zaidi ya 74 yamethibitisha ushiriki wao, akiwaomba Wananchi wenye changamoto Mbalimbali kujitokeza kwa wingi kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha.

Wakili Njohoka amesema Ofisi hizo za Mawakili zilizothibitisha ushiriki wao zina wanasheria wabobezi kwenye Maeneo Mbalimbali ikiwemo kwenye mashauri Ya migogoro ya Ardhi, Mirathi, Makosa ya jinai na kwenye masuala ya biashara na mikataba ya watu binafsi na mikataba ya biashara na kampuni.

Mwenyekiti huyo wa Chama Cha Mawakili kanda ya Arusha amefanya ukaguzi wa maandalizi ya Kliniki hiyo maalum ya kutoa usaidizi wa kisheria kwa wananchi ambapo aliambatana na Mtendaji Mkuu wa Chama chao Wakili Abdillah Mdoe na Mhasibu wa Chama chao Bi. Faudhia Mustapha.

Kuanzia Kesho Mei 08, 2024 Mkuu wa Mkoa wa Arusha kwa siku tatu Mfululizo atakuwa na kliniki maalum ya kusikiliza na kutatua changamoto na kero za wananchi na anasema maandalizi yote yamekamilika, akiahidi pia kutoa Mawakili bure kwa migogoro na kesi mbalimbali zitakazokuwa na uhitaji wa kufikishwa Mahakamani.

Share: