Burundi yafunga mipaka yake baada ya rais wa burundi evariste ndayishimiye kuishutumu rwanda kwamba inawaunga mkono red tabara

Nchi ya Burundi imefunga mipaka yake yote ya ardhini na nchi ya Rwanda kuanzia tarehe 11 Januari 2024.

Waziri wa Mambo ya Ndani Martin Niteretse ametangaza hatua hiyo akiwa mkoani Kayanza Kaskazini mwa Burundi katika mkutano na watawala.

Akiitetea hatua hiyo, Waziri Martin Niteretse amesema, ''Burundi imekuwa na jirani mbaya. Naye ni Paul Kagame, Rais wa Rwanda."

Hatua hii ya Burundi ya kufunga mipaka yake na nchi ya Rwanda inakuja siku chache baada ya Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye kuishutumu Rwanda kwamba inawaunga mkono waasi wa Burundi wa Red Tabara. Hii ni baada ya waasi hao kufanya shambulio katika eneo la mpakani mwa Burundi na DRC na kuwauwa raia wasiopungua 20.

Rais Ndayishimiye aliilaumu Rwanda kwamba imeshindwa kutoa ushirikiano na kukataa kuikabidhi Burundi watu wanaotuhumiwa kuhusika katika jaribio la mapinduzi mwaka wa 2015 na ambao Serikali ya Burundi inadai ndio wamekuwa wanapanga mashambulizi dhidi ya Burundi wakiwa na ngome yao mjini Kigali.

Rwanda imekuwa ikikana kila mara tuhuma hizo dhidi yake na kuchagiza badala yake hali hiyo ya kutoelewana iweze kushughulikiwa katika njia za kidiplomasia.

Awali, Burundi ilifunga mipaka yake na Rwanda mwaka wa 2015 kufuatia tuhuma dhidi ya Rwanda za kuunga mkono jaribio la mapinduzi dhidi ya utawala wa Hayati Rais Pierre Nkurunziza.

Baada ya Rais Evariste Ndayishimiye kuchukua mamlaka mwaka wa 2020, uhusiano kati ya Burundi na Rwanda ulikuwa umeanza kuleta nuru na hivyo mipaka ikafunguliwa tena mwaka wa 2021 na kushuhudia ziara ya kwanza ya Rais Paul Kagame nchini Burundi baada ya miaka zaidi ya 7 ya uhasama mkubwa kati ya mataifa hayo mawili jirani.

Share: