Burkina faso imesimamisha vyombo vya habari vya kimataifa kwa kutangaza ripoti inayolishutumu jeshi la nchi hiyo

Mdhibiti wa vyombo vya habari nchini Burkina Faso amesimamisha vyombo vya habari zaidi vya kimataifa kutokana na kutangaza ripoti inayolishutumu jeshi la nchi hiyo kwa kuua raia.

Serikali ya kijeshi sasa imepiga marufuku mtandao wa Ufaransa TV-Cinq na tovuti za Le Monde na The Guardian, pamoja na shirika la utangazaji la Ujerumani, Deutsche Welle.

Hatua hiyo imechukuliwa siku chache baada ya mamlaka ya Burkinabè kuweka marufuku ya wiki mbili kwa BBC na shirika la utangazaji la Marekani la Sauti ya Amerika (VOA) kwa kuripoti ripoti hiyo hiyo ya Human Rights Watch (HRW).

Baraza la Juu la Mawasiliano (CSC) lilisema katika taarifa yake Jumapili kwamba kuangaziwa kwa ripoti ya HRW na vyombo vipya vilivyositishwa kuendesha shughuli zake huko "kunajumuisha taarifa potofu zinazoweza kuleta kashfa kwa jeshi la Burkina Faso".

Mdhibiti wa vyombo vya habari pia alisisitiza onyo kwa vyombo vyote vya habari dhidi ya kuandika ripoti hiyo, na kutishia kuviwekea vikwazo.

Ripoti hiyo iliyotolewa Alhamisi iliyopita na kundi lenye makao yake makuu nchini Marekani la HRW lilishutumu jeshi la Burkinabè kwa kuwaua takriban raia 223 mwezi Februari kaskazini mwa nchi hiyo.

Mamlaka ya Burkina Faso ilikataa ripoti ya HRW kama "madai yasiyo na msingi" na kusema kuwa wameanzisha uchunguzi wa kisheria "kuthibitisha ukweli".







Share: