Bunge la tanzania kuanza kujadili miswada 3 ya sheria

Bunge la Tanzania limeanza rasmi vikao vyake hii leo huko jijini Dodoma, Tanzania. Vikao hivyo vitakavyodumu kwa muda wa wiki mbili vinatarajiwa kujadili kwa kina mapendekezo yaliyowasilishwa na wadau mbalimbali katika miswada mitatu ambayo ni; Muswada wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge, na Madiwani wa Mwaka 2023, Muswada wa Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi wa Mwaka 2023 na, Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa mwaka 2023.

Mapema mwaka huu, miswada hiyo mitatu iliwasilishwa katika Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria ambapo, kwa muda wa siku nne mfululizo, kamati ilipokea maoni kutoka kwa zaidi ya taasisi elfu moja. 

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk. Joseph Mhagama ingawa alikiri kupokea maoni hayo, na kusema maandalizi yote yamekamilika kwa miswada hiyo kuwasilishwa bungeni katika Mkutano wa 14 wa Bunge, lakini pia alisema sio maoni yote yatawasilishwa kutokana na baadhi ya maoni kutoka nje ya mada. 

Baadhi ya maoni yaliyopendekezwa na wadau, ikiwemo vyama 17 vya kisiasa, asasi za kiraia, viongozi wa dini na wanaharakati wengine ni pamoja na kutaka wakurugenzi wa halmashauri kuondolewa mamlaka ya kusimamia uchaguzi. 

Mbali na hilo, pia kumetolewa pendekezo la kutaka kuondolewa kwa takwa la ushindi wa kura za urais kuwa zaidi ya asilimia 50, pamoja na kuondolewa kwa gharama za kuchukua fomu kwa wagombea. 

Baadhi ya wadau pia wametaka vyama kulazimishwa kuteua asilimia 50 ya wagombea wanawake kwa lengo la kuleta uwiano wa kijinsia katika nyanja mbalimbali za kisiasa.  

Mabadiliko haya yanakuja wakati ambapo serikali ya Tanzania imekuwa ikipata shinikizo kutoka kwa vyama vya upinzani pamoja na wadau wengine wa maendeleo kutaka kuwezesha mchakato wa mabadiliko ya katiba, hasa kipindi hiki ambapo taifa hilo lenye wakazi takriban milioni 60 likijiandaa kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa, na baadae 2025, uchaguzi mkuu, ambao utajumuisha urais, wabunge na madiwani. 

Hata hivyo, rais Samia Suluhu Hassan, mara kadhaa amesikika akisema, kuwa katiba mpya ni mchakato ambao unahitaji wananchi kuwa na elimu ya kutosha ili wajue haki zao za kimsingi na mahitaji yao ya kila siku.

Share: