Bashungwa amemuagiza Meneja wa TANROADS Mkoa Kilimanjaro kuhakikisha magogo, takataka na tope vilivyosambaa katika nyumba hizo na barabara kuu ya Tanga kuelekea Kilimanjaro viondolewe haraka
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amekagua athari za mvua za El-Nino katika mji wa Hedaru na Saweni wilayani Same na kutoa pole kwa Wananchi ambao wameathirika na mvua zilizonyesha usiku na kusababisha maji na tope kujaa kwenye nyumba zao, nyumba za ibada na miundombinu ya barabara.
Akizungumza na wananchi wa maeneo hayo, leo tarehe 24 Novemba 2023, Waziri Bashungwa amemuagiza Meneja wa TANROADS Mkoa Kilimanjaro kuhakikisha magogo, takataka na tope vilivyosambaa katika nyumba hizo na barabara kuu ya Tanga kuelekea Kilimanjaro viondolewe haraka ili Barabara ipitike wakati wote.
Bashungwa amezungumzia umuhimu wa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari wakati mvua zinaendelea kunyesha no katika maeneo hayo na kumtaka Meneja wa TANROADS kuongeza idadi ya wakandarasi ili kazi ya kusafisha mitaro pamoja na kufuatilia mikondo ya maji milimani ili kudhibiti takataka, maji na magogo yasishuke kwa kasi katika makazi ya watu na barabarani.
Aidha, Bashungwa amemtaka Mtendaji Mkuu wa TANROADS, kuwawezesha mameneja wa mikoa ili kukabiliana na athari za mvua zinazoendelea kunyesha ili zisiharibu miundombinu ya barabara na madaraja nchini kote.
Amewataka Mameneja na wataalamu wao kufanya ukaguzi wa maeneo ya madaraja na barabara kila wakati ili kubaini na kudhibiti mapema athari zinazoweza kujitokeza kufuatia mvua hizo.