Somaliland ilijitenga kutoka Somalia tangu mwaka 1991 lakini haitambuliki kimataifa kama taifa huru.
Umoja wa Afrika na Marekani wametoa wito wa kutaka taifa la Somalia kuheshimiwa katika mamlaka yake, tamko hilo limekuja baada mkataba wa bandari wenye utata wa Ethiopia kukubaliwa na Somaliland.
Mkataba huo umesababisha mvutano wa kidiplomasia, huku Somalia ikilaani na kuita ni kitendo cha uchokozi na ukiukaji wa uhuru wake na kuapa kuupinga "kwa njia yoyote ya kisheria."
Somaliland ilijitenga kutoka Somalia tangu mwaka 1991 lakini haitambuliki kimataifa kama taifa huru.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Marekani, Matthew Miller alisema siku ya Jumatano kuwa "Marekani inatambua uhuru na uadilifu wa eneo la Jamhuri ya Shirikisho ya Somalia ndani ya mipaka yake."
Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Moussa Faki pia amehimiza kuheshimiwa kwa "umoja, uadilifu wa eneo na mamlaka ya Somalia na Ethiopia."
Marekani na Umoja wa Afrika pia zimetaka pande zinazohusika kuendeleza mazungumzo ya kidiplomasia ili kutatua mzozo huo kwa amani, huku kukiwa na wasiwasi kwamba makubaliano hayo yanaweza kuzidisha mvutano katika eneo hilo