Kwa Upande wa Zanzibar, Raia wa Ethiopia na Kenya waliongoza kwa kufika visiwani humo
Wizara ya maliasili na utalii imeitaka idara ya wanyamapori kuja na mpango mkakati wa kuongeza idadi ya Twiga na Sheshe, kutokana na wanyama hao kupungua idadi yake na hivyo kutishia kutoweka kwa wanyama hao nchini Tanzania.
Waziri wa Maliasili na Utalii Mh. Angellah Kairuki ametoa kauli hiyo wakati wa Uzinduzi wa Sensa ya wanyamapori na taarifa ya watalii waliofika nchini mwaka 2023, Hafla iliyofanyika Mjini Arusha kwenye ukumbi wa Grand Melia leo Aprili 22, 2024.
Waziri Kairuki pia amezitaka Taasisi na idara za Wizara hiyo kuchakata taarifa zote mbili na kuzichambua, ili ziweze kuwasaidia katika kutimiza majukumu yao ya kila siku katika kulinda maliasili na kukuza utalii.
Waziri Angellah Kairuki pia ametaka kasi zaidi katika udhibiti wa shughuli za kibinadamu kwenye maeneo ya hifadhi pamoja na kuhamasisha suala la utunzaji wa mazingira na kutokukata miti hovyo ili kuendelea kutunza mazingira kwa faida ya viumbehai.
Mh. Kairuki pia amewataka watanzania kuwa Mabalozi wa Utalii kwa kutangaza vivutio vya Utalii vilivyopo nchini ili kuweza kuongeza idadi ya wageni na watalii wanaofika nchini Tanzania.
Katika ripoti iliyozinduliwa leo ya watalii waliofika nchini Tanzania mwaka 2023, ripoti inaonesha kuwa Watalii wengi waliofika nchini Mwaka jana ni wenye Umri wa kuanzia miaka 22-44, huku raia wa Marekani, Italia, Ujerumani wakitajwa kuongoza kuja Nchini Tanzania. Kwa Afrika nchi za Zambia, Kenya na Burundi zimeongoza kwa kuleta wageni wengi zaidi mwaka jana.
Kwa Upande wa Zanzibar, Raia wa Ethiopia na Kenya waliongoza kwa kufika visiwani humo na Ripoti inaonesha kuwa Waliofika Zanzibar kwa wingi walikuwa wanandoa ama Wapenzi wakati kwa Tanzania bara wengi wakitajwa kutokuwa na mahusiano ya kindoa.
Wizara ya Maliasili na utalii inasema lengo la kufanya Sensa ya wanyamapori ni kuhakikisha uhifadhi endelevu ili kutoa takwimu sahihi juu ya uwepo, idadi na mtawanyiko wa wanyamapori pamoja na kudhibiti migogoro kati ya Binadamu na Wanyamapori.