Antony blinken ameiambia israel na hamas wakati ni sasa wa makubaliano ya kuleta usitishaji vita huko gaza

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken ameiambia Israel na Hamas kwamba "wakati ni sasa" wa makubaliano ya kuleta usitishaji vita huko Gaza na kuwaachia huru mateka waliosalia wanaoshikiliwa.

Bw Blinken alisema makubaliano yapo mezani na Hamas wanapaswa kukubaliana nayo.

Wapatanishi wanasubiri jibu kutoka kwa Hamas kwa pendekezo la hivi punde.

Inaripotiwa kuwa makubaliano hayo yanahusisha usitishaji vita wa siku 40 na kuachiliwa kwa zaidi ya mateka 30 wa Israel kwa kubadilishana na wafungwa wengi zaidi wa Kipalestina.

"Tumedhamiria kupata usitishaji mapigano ambao unawaleta mateka nyumbani na kuupata sasa, na sababu pekee ambayo hilo halingeafikiwa ni Hamas," Bw Blinken alisema alipokutana na Rais wa Israel Isaac Herzog mjini Tel Aviv.

"Kuna pendekezo kwenye meza, na kama tulivyosema, hakuna ucheleweshaji, hakuna visingizio. Wakati ni sasa."

Afisa mkuu wa Hamas amekanusha kwamba kundi hilo ndilo linalochelewesha kuafikia makubaliano hayo mapya.

Familia za mateka zilikuwa zikiandamana nje na Bw Blinken akawasalimia, akisema kuwaachilia wapendwa wao ndio "msingi wa kila kitu tunachojaribu kufanya".

Takriban mateka 130 kutoka miongoni mwa 253 waliotekwa nyara na Hamas wakati wa shambulio lisilokuwa na kifani dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba bado hawajulikani waliko.

34 kati yao wanakisiwa kuwa wamekufa. Wengine wameachiliwa au wameokolewa.










Share: