Angola: sonangol imepuuza ripoti kwamba meli iliyolengwa na wapiganaji wa houthi ilikuwa sehemu ya meli zake.

Meli hiyo yenye uhusiano na Uingereza iliwaka moto kwa saa kadhaa Ijumaa iliyopita katika Ghuba ya Aden baada ya kushambuliwa kwa kombora lililorushwa na Wahouthi.

Kampuni ya mafuta inayomilikiwa na serikali ya Angola ya Sonangol imepuuza ripoti kwamba meli iliyolengwa na wapiganaji wa Houthi wiki iliyopita katika Ghuba ya Aden ilikuwa sehemu ya meli zake.

Meli hiyo yenye uhusiano na Uingereza iliwaka moto kwa saa kadhaa Ijumaa iliyopita katika Ghuba ya Aden baada ya kushambuliwa kwa kombora lililorushwa na Wahouthi.

Kundi hilo lenye kuungwa mkono na Iran ambalo makao yake yako Yemen, limesema lililenga meli hiyo kwa jina Marlin Luanda kama hatua ya kujibu "uchokozi wa Marekani na Uingereza".

Taarifa ya kukana kuwa na uhusiano nayo imewadia baada ya vyombo vya habari vya Angola kuhusisha meli hiyo na Sonangol.

"Sonangol inaarifu umma kwamba meli ya Marlin Luanda, iliyoshambuliwa hivi majuzi na kombora katika Bahari ya Shamu, si sehemu ya meli zinazomilikiwa na kampuni au za kukodi," kampuni hiyo ilisema katika taarifa iliyoonekana na vyombo vya habari vya ndani.

Marlin Luanda, inayoendeshwa kwa niaba ya mfanyabiashara wa bidhaa mwenye makao yake Singapore Trafigura, inapeperusha bendera ya Visiwa vya Marshall.

Trafigura ni mmoja wa wasambazaji wakuu wa dizeli na dizeli ya baharini nchini Angola.

Pia ni mbia katika kampuni ya Puma Energy, ambayo inadhibiti vituo vya mafuta vya Pumangol nchini Angola.

Wanahisa wengine katika kampuni ya Puma Energy ni pamoja na Sonangol.

Share: