
Polisi wa jimbo la Texas wamesema mwanaume mmoja anakabiliwa na shtaka la mauaji baada ya tukio la ajabu ambapo yeye na rafiki yake walibadilishana kupigiana risasi kwa kutumia bunduki, huku mmoja wao akijaribu kujikinga kwa kuvaa kofia maalum ya kuzuia risasi (Kevlar helmet).
Kwa mujibu wa taarifa za Polisi wa Kaunti ya Harris, wawili hao—waliotajwa kama Sean Odonnell mwenye umri wa miaka 37 na Aaron Prout mwenye umri wa miaka 34—walifanya jaribio hilo hatari wakiwa nyumbani. Awali, kisa hicho kiliripotiwa kama tukio la kujiua, lakini uchunguzi wa polisi ulibaini kwamba maelezo yaliyotolewa hayalingani na ukweli.
Sheriff Ed Gonzalez alisema tukio hilo lilitokea tarehe 17 Agosti, na askari wanne waliitwa katika nyumba moja iliyopo mitaa ya Pennington Hills. Walipofika, walimkuta mwanaume akiwa amejeruhiwa kwa risasi kichwani. Alikimbizwa hospitalini lakini baadaye alifariki dunia.
Baada ya uchunguzi, polisi walimkamata Odonnell na kumfikisha katika gereza la Kaunti ya Harris. Kwa sasa anashikiliwa kwa dhamana ya dola 300,000 (sawa na shilingi takribani milioni 793 za Kitanzania). Anatarajiwa kufikishwa tena mahakamani Septemba 2. Haijafahamika bado kama amepata wakili au kama ameomba kupewa dhamana rasmi ya kujitetea.