Mahakama ya Ufaransa ilimpata Dominique Pelicot na hatia siku ya Alhamisi ya kumtumia dawa za kulevya na kumbaka mkewe (pichani) mara kwa mara kwa takriban muongo mmoja, na kuwaalika watu wengi wasiowafahamu kubaka mwili wake ambao haukuwa na fahamu katika kesi ambayo imetisha ulimwengu.
Washtakiwa wote 50 wa Mfaransa huyo pia walipatikana na hatia ya ubakaji, jaribio la ubakaji au unyanyasaji wa kijinsia, wakati mwathirika wao, Gisele Pelicot, aliketi katika chumba cha mahakama kilichojaa kusikiliza hukumu hiyo, baada ya kuachilia haki yake ya kutotajwa jina.
Gisele, mwenye umri wa miaka 72, amekuwa ishara ya ujasiri wa kike na ustahimilivu wakati wa kesi hiyo iliyodumu kwa miezi mitatu na umati wa wafuasi wake nje ya mahakama katika mji wa kusini wa Avignon walishangilia alipokuwa akitokea baada ya hukumu kusomwa.
"Kesi hii ilikuwa mtihani mgumu sana," alisema katika maoni yake ya kwanza mwishoni mwa hukumu, na kuongeza kwamba hakujutia uamuzi wake wa kuruhusu kesi hiyo kusikilizwa hadharani.