
Mfanyakazi wa zamani wa kampuni ya akili bandia OpenAI, Suchir Balaji (26), aliyefichua masuala ya ukiukwaji wa hakimiliki yanayohusiana na programu za kampuni hiyo, amekutwa amefariki kwa kujinyonga nyumbani kwake huko San Francisco mwezi uliopita.
Ofisi ya Mchunguzi Mkuu wa San Francisco imethibitisha kifo hicho na kusema kuwa njia ya kifo ilikuwa ni kujiua.
Balaji aliwahi kusema kwenye makala ya The New York Times mwezi Oktoba kwamba alihama kampuni hiyo baada ya kushuhudia changamoto za kimaadili zinazohusiana na mifumo ya AI kama ChatGPT. Aliongeza kuwa mfumo huo hauwezi kuwa na nguvu bila kutawala mfumo wa sasa wa intaneti.
Balaji pia aliweka wazi wasiwasi wake kuhusu matumizi ya kazi za watu wengine bila ridhaa. Taarifa alizokuwa nazo zilitarajiwa kuwa muhimu kwenye kesi dhidi ya OpenAI.