Mwanamke mmoja kutoka Uingereza aitwaye Janet Savage umri wa miaka 54, amefariki dunia baada ya kufanyia upasuaji wa kupunguza mwili kwenda vibaya. Taarifa inasema kwamba Marehemu Janet alisafiri kutoka Uingereza kwenda Uturuki kufanyiwa upasuaji wa kukata utumbo kwa sababu alikuwa anataka kupungua mwili.
Baada ya mwili wa Janet kurudishwa nyumbani na kufanyiwa uchunguzi madaktari waligundua kwamba Janet alifariki kutokana na kuvuja damu nyingi tumboni baada ya mshipa mkubwa wa damu ulioko tumboni kupasuka. Upasuaji wa Janet uligharimu Shilingi Milioni 7,781,400 (Euro 2,750). Watu wengi wanaotaka kufanyiwa upasuaji wa kurekebisha miili yao wamekuwa wakienda Uturuki kutokana na unafuu wa gharama za matibabu au huduma hiyo.
Marehemu Janet amekuwa miongoni wanawake kadhaa wa Uingereza ambao wameripotiwa kupoteza maisha baada ya kwenda kufanyiwa upasuaji huko Uturuki. Inadaiwa kuwa marehemu Janet aliandaa mpango huo mwaka jana Julai na kufanikiwa kwenda mwaka huu mpaka umauti ulipomkuta huko eneo la Ozel Rich katika hospitali binafsi ya Antalya Agosti 5.