Hakimu mmoja jijini Rio de Janeiro, Brazil, ameagiza kufutwa kwa wimbo wa msanii wa Uingereza, Adele, uitwao Million Years Ago kufuatia shtaka la wizi wa kazi ya sanaa lililowasilishwa na msanii wa Brazil, Toninho Geraes.
Geraes anadai kwamba Adele aliiga wimbo wake wa Mulheres, maarufu nchini Brazil tangu miaka ya 1990. Uamuzi huo unalazimisha Sony Music na Universal Music kusitisha mara moja matumizi, usambazaji, au mauzo ya wimbo huo kwenye majukwaa ya kidijitali bila ruhusa ya Geraes, huku faini ya shilingi milioni 19 ikipangwa kwa kutotii agizo hilo.
Hata hivyo, Universal Music imepinga uamuzi huo kwa rufaa, ikisema hakuna wizi, bali kufanana kimuziki kwa bahati mbaya kutokana na matumizi ya vionjo vya kawaida vya muziki.
Toninho Geraes, kupitia mawakili wake, sasa anashirikiana na majukwaa ya muziki kama Spotify na Deezer kuhakikisha wimbo huo unafutwa. Pia, amewasilisha madai ya fidia ya zaidi ya shilingi 350 kwa kukiukwa kwa haki zake za kiubunifu.