ZUCHU ATHIBITISHA KUPOKEA MALIPO YA CHAN BAADA YA MALALAMIKO MTANDAONI

Mwanamuziki wa Tanzania, Zuchu, hatimaye amepokea malipo yake yaliyokuwa yakisubiriwa kufuatia utumbuizaji wake kwenye fainali za CHAN 2024 zilizofanyika Kasarani, Nairobi, tarehe 30 Agosti 2025. Hii imekuja baada ya nyota huyo kulalamika hadharani kuhusu ucheleweshwaji wa malipo yake, jambo lililoibua mjadala mkubwa katika mitandao ya kijamii.

Kwa mujibu wa mkataba wake na LEAP Creative Agency, malipo yalipaswa kufanyika mara baada ya onyesho, lakini Zuchu alidai kuwa alipata usumbufu mkubwa na ucheleweshaji usio na sababu za msingi. Kupitia mitandao ya kijamii, alifichua jumbe na nyaraka za “Proof of Payment” alizopewa, akizitilia shaka kutokana na kutokuwa na uthibitisho wa kweli. Malalamiko yake yalizua mjadala mpana huku mashabiki na wadau wa muziki wakimpa sapoti na kutaka suala hilo lichukuliwe kwa uzito unaostahili.


Zuchu alieleza pia kuwa alilazimika kukataa baadhi ya matamasha mengine ili aweze kutimiza wajibu wake wa kutumbuiza kwenye CHAN, jambo lililoongeza uzito wa madai yake. Baada ya siku chache za shinikizo na sauti yake kusikika, mwimbaji huyo alitangaza kupitia Instagram kwamba amepokea malipo yote aliyokuwa akisubiri. Akiwa mwenye furaha na kutulizwa na hatimaye kuona haki imetendeka, Zuchu aliwashukuru wote waliomsaidia na kumtia moyo katika kipindi hicho kigumu, na kumaliza ujumbe wake kwa maneno mafupi lakini yenye maana kubwa: “Thank you … we move.”

Share: