
Mtayarishaji maarufu wa muziki kutoka Atlanta, Metro Boomin, amekutwa hana hatia katika kesi ya madai ya unyanyasahi wa kingono iliyokuwa ikimkabili.
Uamuzi huo ulitolewa Alhamisi, Septemba 25, baada ya shauri lililodumu siku tatu, ambapo baraza la majaji lilihitaji chini ya saa mbili pekee kufikia hukumu ya kumtoa Metro kwenye mashitaka yote manne yaliyokuwa yamefunguliwa dhidi yake, yakiwemo ubakaji, unyanyasaji wa kingono, ukiukaji wa Ralph Act, na ukatili wa kijinsia.
Akizungumza mara baada ya uamuzi huo kutolewa, Metro alionyesha furaha yake kwa matokeo hayo, akisema anajiona mwenye baraka na kwamba ukweli hatimaye umeibuka. Alimshukuru pia msanii Young Thug kwa kujitokeza mahakamani kumpa msaada wakati wa kusikilizwa kwa shauri hilo.
Kesi hiyo ilifunguliwa mwaka jana na Vanessa LeMaistre, aliyedai kwamba mwaka 2016 Metro alimlazimisha kufanya naye ngono katika hoteli moja mjini Las Vegas wakati akiwa hana fahamu baada ya kupewa dawa ya Xanax na pombe. LeMaistre alidai pia kuwa alibeba ujauzito kutokana na tukio hilo lakini aliutoa. Baada ya majaribio ya kufikia makubaliano ya kifedha kugonga mwamba mapema mwaka huu, kesi iliendelea mahakamani kuanzia Septemba 23, ambapo wote wawili walitoa ushahidi.
Wakili wa Metro, Lawrence Hinkle, aliwaeleza majaji kwamba madai hayo hayakuwa na ukweli wowote bali yalikuwa jaribio la kupata pesa kwa urahisi. Alisisitiza kuwa mlalamikaji alidhani mteja wake angekubali kulipa ili kumaliza jambo hilo kimya kimya, jambo ambalo halikutokea.
Kwa uamuzi huu, Metro Boomin anaendelea kuwa huru kisheria huku akipongezwa na mashabiki wake kwa kusimama imara wakati wa kipindi kigumu cha maisha yake.